The House of Social Media
gunners X

Taarifa ya Polisi Kuhusu Kundi la Uasi Mwanza – Video

0

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa wananchi kuzipuuza taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zenye kichwa cha habari kinachodai kuwa “kundi la uhasi laibuka Mwanza, Polisi waonekana mitaani.”

Jeshi hilo limeeleza kuwa hali ya usalama katika Mkoa wa Mwanza ni shwari, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema askari wake wanaendelea kutimiza majukumu yao ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, taarifa hizo ni za upotoshaji na zinasambazwa kwa lengo la kuleta taharuki katika jamii. Limeeleza kuwa wahalifu wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii wamekuwa wakichukua picha za askari Polisi na vitendea kazi vyao kisha kutengeneza maudhui yenye lengo la kuzua taharuki, kuchonganisha na kupandikiza chuki miongoni mwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limewasisitiza wananchi kuendelea kuwapuuza watu wanaosambaza taarifa zenye nia ovu na badala yake wafuatilie na kupata taarifa sahihi na za kweli kutoka kwenye mamlaka zenye jukumu la kutoa taarifa hizo.

Vilevile, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea kuwafuatilia kwa karibu watu wote wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo, uchonganishi na zinazopandikiza chuki kwa jamii, kwani vitendo hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Leave A Reply