
Rais wa Marekani Donald Trump ameibua mjadala mkubwa kimataifa baada ya kumkejeli Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kurejea tukio la zamani lililomhusisha mkewe, Brigitte Macron.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha Pasaka, Trump alitoa kauli ya mzaha akidai kuwa Macron “bado hajapona” baada ya tukio la video iliyosambaa mwaka jana, iliyomuonyesha akiguswa kwa nguvu usoni na mkewe wakati wakijiandaa kushuka kwenye ndege huko Hanoi, Vietnam.

video inayomuonyesha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akipigwa kofi na mkewe, Brigitte Macron, wakati wakijiandaa kushuka kwenye ndege jijini Hanoi, Vietnam.
Katika hotuba hiyo, Trump alisema:
“Nilimpigia simu Macron ambaye mkewe anamtendea vibaya bado anauguza pigo la usoni.”
Kauli hiyo ilionekana kuwashangaza wengi na kuzua ukosoaji, hasa kutokana na uzito wa masuala ya kimataifa yanayoendelea kwa sasa.
Akijibu kauli hiyo akiwa ziarani nchini Korea Kusini, Macron alionyesha kutoridhishwa na matamshi ya Trump, akiyataja kuwa hayakuwa ya kiungwana wala ya kiwango kinachotarajiwa kutoka kwa kiongozi wa dunia.
Macron alisema: “Tunahitaji kuzungumzia mambo mazito kama vita na maisha ya watu. Kauli kama hizi si za heshima na hazistahili hata majibu.”

Mvutano huu wa maneno unakuja wakati hali ya kisiasa duniani ikiwa tete, hasa kutokana na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati. Katika hotuba hiyo hiyo, Trump alitoa msimamo mkali dhidi ya Iran, akitishia kuchukua hatua kali za kijeshi endapo hali katika eneo la Strait of Hormuz haitaimarika.
Mbali na hilo, Trump aliendelea kuikosoa NATO, akidai washirika wake hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa Marekani. Aidha, aligusia uwezekano wa Marekani kujiondoa katika muungano huo wa kijeshi.
Hatua hiyo, ikiwa itachukuliwa, inaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa kimataifa, kwani Marekani ni mhimili mkuu wa nguvu za kijeshi ndani ya NATO.
Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mgogoro mkubwa katika historia ya muungano huo, huku nchi wanachama zikilazimika kutafuta mbinu mbadala za kujilinda bila msaada mkubwa wa Marekani.
