Leo katika safu hii tunakutana na Video Queen, Hanaiyah Abdallah. Ni mrembo aliyeuza nyago katika video nyingi za muziki kama vile Togola Mama ya Dully Sykes, Siachani Nawe ya Barakah Da Prince na nyingine kibao.
Kupitia Mwandishi Wetu, Nyemo Chilongani utafahamu mengi usiyoyajua kuhusu binti huyu mwenye macho makubwa ya kurembua, ngozi yake kama Muarabu f’lani hivi kupitia maswali 10 aliyoulizwa.
Ijumaa: Kwa nini unaitwa Baby Annahiyah?
Baby: Kitu cha kwanza nilianza kujitazama mimi kama mimi, jinsi nilivyo ni mrembo, najikubali basi kwa kuwa niliona hivyo, nikaamua kujiita Baby Annahiyah na kweli jina hilo limekubalika.
Ijumaa: U msichana mrembo sana, maisha yako ya nyuma vipi? Una mpenzi?
Baby: Hapana! Kwa kweli kwa sasa nipo singo, sina mtu yeyote yule. Nilikuwa naye mwaka jana lakini tukagombana na kila mtu kuishi maisha yake japokuwa tunawasiliana kama marafiki.
Ijumaa: Ulishawahi kudate na supastaa?
Baby: Hahaah! Ni swali gumu sana kulijibu, naomba iwe siri yangu.
Ijumaa: Ulimpendea nini aliyekuwa mpenzi wako?
Baby: Alikuwa mtu wa kujali, kusikiliza na kuheshimu. Japokuwa kulikuwa na mambo mengine, ila hivyo vilikuwa vitu pekee nilivyovipenda.
Ijumaa: Ushawahi kuchukuliwa vibaya na jamii kutokana na fani yako ya U-Video Queen?
A: Ndiyo! Hiyo hutokea, tena mara nyingi. Unajua watu wengi uwezo wao wa kufikiria ni mdogo. Mwingine akikuona kwenye video ya mtu, anajua kwamba ni lazima utoke na huyo mtu.
Ijumaa: Nini unakipenda katika kazi yako?
Baby: Napenda kupendeza, kulipwa vizuri na kuifanya video husika iwe bora.
Ijumaa: Kwa nini hupendi kujichora tatuu kama wafanyavyo wenzako wengi?
Baby: Wengi wananiuliza swali hilo ila jibu lake ni jepesi tu kwamba dini yangu haikubali na pia mama yangu hapendi mambo ya matatuu, hivyo sipendi kumkwaza.
Ijumaa: Kitu gani kiliwahi kukuumiza?
Baby: Nakumbuka kuna siku nilikuwa na dola elfu mbili (zaidi ya milioni nne). Nilimwambia mama, akaniambia nimpe aniwekee, nikakataa. Sasa siku hiyo nikawa nakwenda klabu na marafiki zangu, nikachukua dola 500 na kuweka kwenye kipochi changu. Baadaye sijui nini kilitokea, fedha zile zikuziona na marafiki wenyewe wakawa wanajikanyagakanyaga kila nilipowauliza. Nikajua walihusika. Iliniuma sana.
Ijumaa: Gharama yako katika video ipo vipi?
Baby: Gharama yangu, kwa mastaa napokea mpaka laki saba, nane na wakati mwingine mpaka milioni moja. Kwa underground, huwa juu zaidi kwani naamini sura hii ikiwa kwenye video, itavuta watazamaji wengi. Hivyo wanatakiwa kuilipia gharama zaidi.
Ijumaa: Mama yako anafurahi kukuona kwenye video?
Baby: Kwa sasa anakubaliana nami baada ya kukubali kwamba hii ni ajira ila awali hakupenda.