
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza adhabu kwa klabu kadhaa za Ligi Kuu Tanzania kutokana na makosa mbalimbali yaliyotokea katika michezo ya hivi karibuni.
Katika maamuzi yaliyotolewa leo Aprili 20, 2026 kufuatia kikao kilichofanyika Aprili 18, klabu ya Simba SC pamoja na TRA United zimetozwa faini ya Tsh milioni 5 kila moja. Adhabu hiyo imetokana na tukio la vurugu lililohusisha walinzi wa klabu hizo (stewards) kupigana mara baada ya timu hizo kuwasili katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Stadium kabla ya mchezo wao uliomalizika kwa sare tasa.
Aidha, klabu ya Azam FC nayo imetozwa faini ya Tsh milioni 5 kwa kosa la viongozi wa benchi la ufundi na wachezaji kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani, kinyume na kanuni za Ligi Kuu na makubaliano ya kikao cha maandalizi ya mchezo wa Dabi ya Mzizima.
Katika hatua nyingine, Simba SC imetozwa faini ya Tsh milioni 10 baada ya baadhi ya mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili katika mchezo wa Dabi ya Mzizima uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex na kumalizika kwa sare tasa. TPLB imesema tukio hilo ni la kujirudia kwa klabu hiyo msimu huu, jambo lililopelekea adhabu kuongezwa.
TPLB imesisitiza kuwa hatua hizi zinalenga kuimarisha nidhamu, usalama na uendeshaji bora wa ligi, huku ikitoa onyo kwa klabu zote kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuepuka adhabu zaidi.
