×

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Apokea Tuzo Kutoka kwa Wafanyabiashara Kariakoo

Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) imemtunuku tuzo maalumu Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya biashara jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilikabidhiwa rasmi na Mwenyekiti wa JWK, Sevein Mushi, wakati wa Mkutano Mkuu wa jumuiya hiyo uliofanyika katika Soko Kuu la Kariakoo.

Mwenyekiti Mushi alisema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya kutambua juhudi kubwa alizozifanya Mpogolo katika kusimamia na kukuza biashara katika eneo la Kariakoo, ambalo ni kitovu kikubwa cha biashara jijini. Alitaja moja ya mafanikio makubwa ya Mpogolo ni hatua alizochukua katika kufungua barabara na mitaa ya soko hilo, jambo ambalo limeongeza urahisi wa biashara na kupunguza msongamano katika maeneo ya biashara.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo, alishukuru wafanyabiashara kwa heshima hiyo kubwa waliyo mpa. Alisema kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Mpogolo alisisitiza kuwa Rais Samia ameendelea kufungua fursa za kiuchumi ambazo zimejenga mazingira bora kwa wafanyabiashara na kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika uchumi wa taifa.

“Tunatambua juhudi kubwa za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza fursa za kiuchumi na kutekeleza miradi mikubwa ambayo imewezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa urahisi zaidi. Tuzo hii ni motisha kwetu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujitolea katika kuleta maendeleo,” alisema Mpogolo.

Kariakoo, ambayo ni soko kuu la biashara jijini Dar es Salaam, imekuwa ni mojawapo ya maeneo muhimu yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa mkoa wa Dar es Salaam na taifa kwa ujumla. Tuzo hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanaboreshwa na kuwa na ufanisi zaidi.

Leave a Comment