
Rais wa Tanganyika Law Society (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema chama hicho kina wajibu mkubwa si tu kwa wanachama wake bali pia kwa jamii, Serikali na mhimili wa mahakama katika kuhakikisha haki inatendeka, sheria zinaheshimiwa na misingi ya utawala bora inalindwa.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa TLS, TLS AGM 2026, Mwabukusi alisisitiza kuwa jukumu la mawakili limejikita katika sheria, na kwamba wanapotekeleza wajibu wao wa kutoa msaada wa kisheria kwa watuhumiwa mahakamani hawapaswi kutishwa wala kushambuliwa.
Alionya dhidi ya vitisho au mashambulizi kwa mawakili na TLS kwa kutekeleza majukumu yao ya kisheria, akisisitiza kuwa hilo ni sehemu ya kulinda haki na utawala wa sheria.
Aidha, aliwapongeza TLS pamoja na mawakili waliotoa mchango wao katika kutetea wananchi katika kesi nzito zikiwemo za uhaini na unyang’anyi wa kutumia silaha, akieleza kuwa wamefanya kazi kwa bidii kuhakikisha haki inatendeka.

