
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania TASAC limethibitisha kifo cha baharia raia wa Tanzania, Macha Maregesi Mongu, baada ya meli aliyokuwa akifanyia kazi kushambuliwa kwa bomu katika Mfereji wa Hormuz.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo limetokea Mei 3, 2026 wakati marehemu akiwa anahudumu katika meli ya kuvuta (tug boat) iitwayo VOLANS, yenye namba ya usajili wa Shirika la Bahari Duniani (IMO 929856), iliyokuwa ikipeperusha bendera ya United Arab Emirates. Meli hiyo ilikuwa safarini kutoka UAE kuelekea Oman.
TASAC imesema meli hiyo ilishambuliwa wakati ikipita katika eneo la kimkakati la Mlango Bahari wa Hormuz, eneo linalojulikana kwa umuhimu wake mkubwa katika usafirishaji wa mafuta duniani na pia kwa mvutano wa kiusalama.
Katika taarifa yao, TASAC imetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, ikiungana nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Shirika hilo pia limesema linafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha mwili wa marehemu unarejeshwa nchini mara utakapopatikana.
Aidha, TASAC imesisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya mabaharia wanapokuwa baharini, hasa katika maeneo yanayohusisha haki ya kupita kwa amani (innocent passage), kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS).
Kwa sasa, uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea huku macho yakielekezwa katika usalama wa baharini katika eneo hilo lenye mvutano mkubwa wa kimataifa.
