
DAR ES SALAAM, Tanzania – 4 Mei 2026. Kama kinara wa huduma za kifedha Afrika Mashariki, Benki ya KCB imejipanga kuchochea ukuaji wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya, ikilenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya mataifa yote mawili. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank Group, Paul Russo kupitia jukwaa la kibiashara kati ya Tanzania na Kenya lililozinduliwa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan akiongozana na Rais wa Kenya, William Rutto.
Katika mkutano huo, Paul Russo alisema, “Ushiriki wetu unasisitiza dhamira ya benki yetu ya KCB kuwa mshirika wa kuaminika katika kukuza maendeleo ya kikanda na mshikamano wa kiuchumi. Tunajivunia kuwa mstari wa mbele katika kuunganisha wafanyabiashara na viongozi wa sera ili kufungua uwezo kamili wa soko la Afrika Mashariki.”
Kwa upande wa marais, wamedhamiria kudumisha amani na mshikamano baina ya nchi zote mbili ambapo kwa pamoja wameweka nia ya kuunganisha mabaraza ya biashara ya Tanzania na Kenya ili kuunda umoja wa baraza la kibiashara litakaloharakisha mchakato wa muunganiko kati ya nchi hizi mbili.

Benki ya KCB imedhamiria kuimarisha nafasi yake kama daraja la kibiashara Afrika Mashariki kupitia ufadhili wa Biashara (Trade Finance) ili kurahisisha miamala ya mipakani, kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa makampuni ili kusaidia uwekezaji mkubwa wa viwanda na miundombinu na kutoa suluhisho za muunganiko wa kifedha kwa wateja wa ukanda mzima.
Aidha katika mjadala huo, mambo mengi muhimu yalijadiliwa pamoja na: fursa kubwa ambazo bado hazijatumika kati ya Tanzania na Kenya; hatua za kisera za serikali zinazoweza kuharakisha ushiriki wa sekta binafsi; dira ya miaka 10 ya biashara katika ukanda huo; na namna ya kuunda ushirikiano wa kibiashara unaoweza kunufaika kikamilifu la eneo huru la biashara la bara la Afrika.