
Mshawishi maarufu wa mtandaoni Ashly Robinson maarufu kama Ashlee Jenae, aliyefariki ghafla akiwa safarini nchini Tanzania, Aprili 9, 2026 katika hoteli ya Zuri, Nungwi- Zanzibar tukio lililoacha maswali mengi na majonzi makubwa kwa familia na mashabiki wake.
Mchumba wake, Joe McCann, anadaiwa kupitia kipindi kigumu kutokana na vitisho na mashambulizi ya maneno kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na TMZ, Joe na familia yake wamekuwa wakipokea ujumbe wa chuki, vitisho vya kuuawa pamoja na kauli za kibaguzi tangu kifo cha Ashlee kilipotokea.

Vyanzo vilivyo karibu na Joe vimedai kuwa shutuma zinazomhusisha na kifo cha Ashlee zimemuumiza sana kihisia, hasa kutokana na madai yanayosambazwa mtandaoni yakimtuhumu kuhusika na tukio hilo bila ushahidi rasmi kutoka kwa mamlaka.
Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa baadhi ya watumiaji wa mitandao wamekuwa wakitoa maoni ya kibaguzi kuhusu uhusiano wa wawili hao, huku wakieneza simulizi zinazomlenga Joe kama mwanaume mzungu mwenye uwezo mkubwa wa kifedha aliyemuua mchumba wake mwenye asili ya Kiafrika-Amerika.
Vyanzo hivyo vinasisitiza kuwa Joe alimpenda Ashlee kwa dhati na amekuwa tayari kushirikiana kikamilifu na vyombo vya uchunguzi tangu tukio hilo litokee.
Kwa upande wa uchunguzi, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa polisi awali walihisi huenda kifo hicho kilikuwa ni kujiua, ingawa hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kubadilisha au kuthibitisha hitimisho hilo. Hata hivyo, familia ya Ashlee imeeleza kuwa wana mashaka makubwa kuwa binti yao angeweza kuchukua uamuzi wa kujidhuru.
Joe, ambaye alidaiwa kumvisha pete ya uchumba Ashlee wakati wa safari hiyo nchini Tanzania, alihojiwa na mamlaka baada ya tukio hilo na pasipoti yake kushikiliwa kwa muda kwa ajili ya uchunguzi. Hata hivyo, hajakamatwa wala kushtakiwa kuhusiana na kifo hicho.