
Akaunti ya TikTok ya Msanii na mtunzi wa nyimbo kutoka Marekani, D4vd imeondolewa kwenye platform hiyo wiki chache baada ya kukabiliwa na mashtaka makubwa ya mauaji ya Celeste Rivas Hernandez.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ukurasa wake wa TikTok haupatikani tena ambapo watumiaji wanaojaribu kuutafuta hukutana na ujumbe unaoonyesha akaunti hiyo imefungiwa.

Inaelezwa kuwa hatua hiyo inaweza kuwa imechukuliwa kutokana na sera za TikTok zinazopinga maudhui yanayohusiana na vurugu pamoja na tabia zinazokiuka miongozo ya jamii ya platform hiyo.
Hii si mara ya kwanza kwa D4vd kuchukuliwa hatua na mitandao ya kidijitali, kwani awali muziki wake uliondolewa mfumo wa mapato wa YouTube kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni tabia zake nje ya platform zinazokiuka sera za jamii ya YouTube.

Aidha, ripoti zinaeleza kuwa msanii huyo aliachwa kimyakimya na kampuni yake ya muziki baada ya polisi kuanza kumhusisha na uchunguzi wa mauaji ya Celeste.
D4vd alifikishwa mahakamani mwishoni mwa Aprili akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya daraja la kwanza, unyanyasaji wa kingono pamoja na kuharibu mwili wa binadamu.
Mashtaka hayo yanahusishwa na tukio la kupatikana kwa mwili wa Celeste mwenye umri wa miaka 14 ukiwa umekatwa vipande ndani ya gari aina ya Tesla linalodaiwa kuhusishwa na msanii huyo.
Hata hivyo, D4vd amekana mashtaka yote dhidi yake na kwa sasa anashikiliwa gerezani Los Angeles bila dhamana huku uchunguzi ukiendelea.