×

Airtel Africa Yavuna Mabilioni Kupitia Data na Airtel Money

Matumizi ya intaneti (data) na huduma za fedha kupitia simu yamekuwa injini kuu ya ukuaji wa mapato ya Airtel Africa, huku kampuni hiyo ya mawasiliano ikitangaza ongezeko kubwa la mapato na faida kwa mwaka ulioishia Machi 31, 2026, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kidijitali katika masoko yake 14 Afrika.

Kampuni hiyo imesema faida halisi imepanda zaidi ya mara mbili hadi dola milioni 813 kutoka dola milioni 328 mwaka uliopita, ikiwa imechangiwa na ongezeko la mapato ya uendeshaji na faida za ubadilishaji wa fedha za kigeni.

Mapato yamepanda kwa asilimia 29.5 hadi dola bilioni 6.42 kwa thamani ya ripoti, huku ukuaji wa sarafu thabiti ukiwa asilimia 24.

Airtel Africa imesema mafanikio haya yamechochewa zaidi na ongezeko kubwa la matumizi ya data na huduma za Airtel Money, vinavyoendelea kubadili muundo wa mapato yake na kuongeza matumizi ya wateja.

Mkurugenzi Mtendaji, Sunil Taldar, amesema matokeo haya yanaonyesha “msingi imara wa biashara na utekelezaji wenye nidhamu,” akibainisha kuwa matumizi ya huduma za kidijitali na uwekezaji wa mtandao ni nguzo kuu za ukuaji wa kampuni.

“Mkakati wetu umeleta ongezeko la rekodi la wateja, mapato na faida kabla ya kodi na riba (EBITDA),” amesema Taldar. “Data na huduma za fedha mtandao ni injini muhimu ya ukuaji wetu katika kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali barani Afrika.”

Idadi ya wateja wa Airtel Africa imeongezeka kwa asilimia 10.5 hadi milioni 183.5, ikiwa ni ongezeko kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa na kampuni hiyo. Wateja wa huduma za data wamefikia milioni 84.2, huku matumizi ya simu janja yakipanda hadi asilimia 49.5, jambo lililochochea ongezeko la matumizi ya data.

Matumizi ya data kwa kila mteja yameongezeka hadi GB 8.9 kwa mwezi kutoka GB 7.0 mwaka uliopita. Mapato ya data yamepanda kwa asilimia 35.2 kwa sarafu thabiti, na kuifanya kuwa chanzo kikuu cha mapato ya kampuni.

Huduma za Airtel Money nazo zimeendelea kukua kwa kasi, ambapo wateja wameongezeka kwa asilimia 21.3 hadi milioni 54.1. Thamani ya miamala kwa mwaka imepanda kwa asilimia 49 na kufikia zaidi ya dola bilioni 215 katika robo ya nne ya mwaka wa fedha.

Kampuni imesema mapato ya Airtel Money yameongezeka kwa asilimia 28.4 kwa sarafu thabiti, yakichochewa na matumizi ya malipo ya kidijitali, huduma za wafanyabiashara na miamala ya kimataifa.

Faida kabla ya riba, kodi na makato (EBITDA) imepanda kwa asilimia 30.4 kwa sarafu thabiti hadi dola bilioni 3.16, huku kiwango cha faida kikifikia asilimia 49.3 kutokana na udhibiti wa gharama na ukuaji wa mapato.

Airtel imesema ongezeko la matumizi ya data na huduma za fedha limeisaidia kampuni kukabiliana na changamoto za mfumuko wa bei na mabadiliko ya sarafu katika baadhi ya nchi, hususan Nigeria.

Faida ya uendeshaji imepanda kwa asilimia 45.1 hadi dola bilioni 2.12, huku faida kwa hisa moja (EPS) ikipanda hadi senti 18.6 kutoka senti 6.0 mwaka uliopita.

Uwekezaji wa mtaji umeongezeka kwa asilimia 31.9 hadi dola milioni 884, ukiwa umeelekezwa katika upanuzi wa mtandao, ikiwemo ujenzi wa zaidi ya vituo 3,250 vipya na kuongeza kilomita 3,200 za nyaya za fiber.

Airtel inatarajia kuongeza uwekezaji hadi takribani dola bilioni 1.1 mwaka wa fedha 2027 ili kuimarisha miundombinu ya kidijitali na huduma za mtandao wa kasi.

Mtandao wa 4G sasa unapatikana katika asilimia 98.5 ya vituo vyote, huku zaidi ya vituo 3,100 vya 5G vikiwa vinafanya kazi katika masoko sita.

Taldar amesema teknolojia ya akili bandia (AI) na kidijitali imeboresha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa ndani ya kampuni kupitia matumizi ya programu ya MyAirtel.

Airtel Money na huduma za data zimeendelea kuwa nguzo kuu za ukuaji wa kampuni, huku mkakati ukiwa ni kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kidijitali barani Afrika, ambapo kiwango cha upatikanaji wa huduma za benki bado ni cha chini.

Kampuni pia inaendelea kupanua ushirikiano wa kimkakati, ikiwemo mradi wa mawasiliano ya satelaiti na SpaceX kupitia Starlink Direct-to-Cell, unaolenga kufikisha huduma katika maeneo ya vijijini yasiyo na mtandao wa kawaida.

Airtel Africa inaendelea kuwa na mtazamo chanya wa ukuaji licha ya shinikizo la gharama za nishati, ikibainisha kuwa mahitaji ya huduma za kidijitali bado yako juu katika masoko yake.

Leave a Comment