×

Christian Bella: Aandamwa na usalama wa taifa, agombana na Totoo Ze Bingwa

1 (1)

Wiki iliyopita Christian Bella ‘Obama’ alielezea namna alivyomshuhudia mkewe wakati akijifungua mtoto wao wa kiume aitwaye Hance. Kitendo hicho alisema ndiyo ilikuwa sababu kubwa iliyosababisha yeye kupata ‘idea’ ya Wimbo wa Nani Kama Mama. Akaendelea kuwa, baada ya ishu hiyo kupita alielekea nchini Marekani alikokaa kwa muda wa mwaka mmoja na zaidi.
Akiwa Marekani Bella anasema alianza kufikishiwa maneno na washkaji zake waliokuwa Bongo kuwa kuna tetesi zilikuwa zinaendelea kwamba maisha yalimshinda Bongo akaamua kutelekeza chumba chake alichokuwa anaishi na kutimkia ughaibuni kusaka maisha!
Je, nini kiliendelea? Tiririka nayo…

BELLA anasema maneno hayo hayakumuumiza kichwa sana kwa maana alikuwa anafahamu alichokuwa anakifanya. Anasema baada ya muda wake aliokuwa amepanga kukaa Marekani kumalizika alirejea tena nchini Sweden alikokuwa mkewe na mwanaye Hance.

Akiwa Sweden Bella anasema alitunga wimbo uitwao Msaliti na baada ya kuurekodi aliutuma kwenye media mbalimbali Bongo, jambo ambalo hakulitegemea anasema ni jinsi wimbo huo ulivyotokea kukubalika zaidi kwa wapenzi wengi wa muziki bila hata ya kuufanyia ‘promo’ wala ‘media tour’.
Hata aliporejea Bongo kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake za kimuziki Bella anasema kutokana na jina lake kuendelea kuwa kubwa alialikwa kwenye matamasha ya Fiesta yanayoandaliwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM, akiwa msanii pekee wa dansi aliyezunguka karibia mikoa yote nchini akiwaburudisha wapenzi wa kazi zake.
“Hivyo ndivyo nilivyozidi kuwa mkubwa kwenye industry, nafikiri viongozi wa Akudo waliliona suala hilo maana baada ya kumaliza mizunguko ya Fiesta walinifuata wakitaka nirudi tena kwenye bendi yao kutokana na ukweli kuwa ilikuwa imeanza kupoteza stamina.

“Lakini sikuweza kukubaliana na suala hilo kwa sababu tayari nilikuwa nina mipango yangu mingine ambayo sikuhitaji kabisa kurudi nyuma wala mtu yeyote anikwamishe kwenye mipango hiyo,” anasema Bella.

Anaongeza kuwa mwanzoni hakufahamu kuwa kukataa kwake kurudi tena Akudo lilikuwa ni suala ambalo lilimjengea chuki na uadui wa chinichini na watu wa bendi hiyo. Bila kutegemea baadaye alianza kuandamwana na watu wa usalama wa taifa wakidai alikuwa anaishi nchini kinyume na sheria, yaani hakuwa na vibali.
Bella anaendelea kuelezea kuwa madai hayo ‘aliyasovu’ kwa kufikisha kwenye idara husika ya usalama wa taifa vielelezo vyake vya makazi na uhalali wa kuishi nchini, ishu nzima baadaye ikaisha, anasema ingawa aliwagundua watu waliokuwa wanamchoresha, aliamua kuwasamehe na kuendelea na ishu zake.

“Nilijikita kwenye suala zima la kuanzisha bendi yangu, Mungu alisaidia Novemba 2013 kama sikosei ilikuwa ni tarehe 15, tuliizindua bendi kwenye Ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama huku tukitambulisha kwa kuanza nyimbo mbili ambazo ni Nakuhitaji na Mtu wa Watu.

“Kwenye bendi nina vichwa vikali wakiwemo Adaya, Petit Mauzo, Pilu, Mico Bella, Chesco Vuvuzela, Yanick Soslo, Babu Bomba, Kadogoo Machine na msaidizi wangu nilimteua rapa Toto Ze Bingwa,” anasema Bella.

Anaendelea kuwa kama ilivyokuwa awali kutopenda kitendo cha wasanii wa bendi kufanya maonesho zaidi ya mara tatu kwa wiki tena kwenye manispaa moja suala ambalo yeye binafsi alifikiri kuwa ndilo lilikuwa linachangia kuua vipaji na kuiporomosha kwa kiasi kikubwa tasnia ya muziki huo, kwenye bendi yake aliweka utaratibu mzuri wa kufanya matamasha suala ambalo aliamua kuliweka wazi bendini kila mmoja akalifahamu.

Siku ziliendelea kusonga mbele Bella anasema katika hali ambayo hakuitegemea kabisa mara iliibuka sintofahamu kwenye bendi yake, ambapo ishu nzima baada ya kuvuja nje hali ya sintofahamu iliongezeka na vyombo vya habari vikaanza kumuandama ili kuona kama vitaambulia kuufahamu ukweli.

“Ishu nzima ilikuwa inanihusu mimi na msaidizi wangu Toto Ze Bingwa kuwa tulikuwa na bifu zito lililosababisha hata asionekane kwenye matamasha tuliyokuwa tunayafanya.
Je, nini kiliendelea? Usikose Jumamosi ijayo hapahapa.

Leave a Comment