×

Serikali Yatangaza Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Hamad Masauni.

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imetangaza rasmi ratiba ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yatakayofanyika kitaifa kuanzia Mei 11 hadi Juni 5, 2026, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”

Tamko hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Hamad Masauni.

Katika hotuba yake, Masauni amesema maadhimisho ya mwaka huu yanakwenda sambamba na kaulimbiu ya kimataifa inayosema “Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Vitendo,” ambayo inalenga kuhimiza hatua za haraka katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira kupitia kampeni za upandaji miti, matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za mazingira.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, huku zaidi ya asilimia 76 ya miti iliyopandwa mwaka 2025/26 ikitajwa kustawi.

Masauni amesema Tanzania pia inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la taka ngumu, ambapo nchi huzalisha kati ya tani milioni 12.1 hadi 17.4 za taka kwa mwaka, kiwango kinachotarajiwa kuongezeka kufikia tani milioni 60 ifikapo mwaka 2050.

Katika kuelekea maadhimisho hayo, Serikali imepanga shughuli mbalimbali ikiwemo:

  • Kongamano la vijana kuhusu mazingira katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mei 26, 2026
  • Maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
  • Maonesho ya teknolojia na ubunifu wa mazingira jijini Dodoma.
  • Uzinduzi wa Kituo cha Afrika cha Vijana kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
  • Hafla ya kilele Juni 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, Dodoma, Juni 05, 2026.

Katika hafla hiyo shughuli zitakazofanyika ni pamoja na: Uzinduzi wa Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania (2026 – 2030), Programu hii ni nyenzo mahsusi ya kuwezesha utekelezaji wa Dira 2050 hususan nguzo inayohusu hifadhi ya mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi; na utoaji wa Tuzo za Maalum kwa wadau kutambua mchango wao katika Uhifadhi wa mazingira.

#PART 2: UNDANI wa USHAHIDI ULIOMTIA HATIANI ‘MR BLUE’ na KUHUKUMIWA KUNYONGWA kwa KUMUUA EZENIA

Leave a Comment