×

The Begining of My End (Mwanzo wa Mwisho wangu-03)

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.
Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.
Historia ya makuzi ya Ben, inamfanya Jordan ahisi kwamba Ben hajaua ila ameamua kukubali kwa sababu ambazo yeye mwenyewe ndiye anayezijua. Jitihada zake za kutaka kuufahamu ukweli ili amnasue rafiki yake huyo kutoka kwenye kitanzi kilichokuwa kinamsubiri, zinagonga mwamba kutokana na Ben kukataa kutoa ushirikiano, muda wote aking’ang’ania kwamba ni yeye ndiye aliyeua.
Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.
Je, nini kitafuatia? Ben atapewa hukumu gani? SONGA NAYO…
Tofauti na wengi walivyotegemea kwamba ataanza kujitetea, Ben aliinua uso wake huku tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake. Akamtazama jaji aliyekuwa amemkodolea macho, akahamisha macho na kumtazama wakili aliyekuwa anamtetea, Jordan, akahamisha tena macho na kuyatuliza kwa mkewe ambaye alikuwa amejiinamia, machozi yakiendelea kumbubujika kama chemchemi ya maji.
“Ndugu mshtakiwa, una lolote la kujitetea kabla sijasoma hukumu?” jaji alirudia swali lile lakini kama ilivyokuwa awali, Ben hakujibu chochote zaidi ya kuendelea kumtazama mkewe na mwanaye.
“Mheshimiwa jaji, naomba mteja wangu apunguziwe adhabu kwa sababu hili ni kosa lake la kwanza, hana historia ya kufanya tukio kama hili. Isitoshe ana mke na mtoto mdogo ambao wote wanamtegemea kama unavyowaona hapo mbele yako mheshimiwa.
Pia afya ya mteja wangu siyo nzuri kama unavyomuona, amedhoofika kwa sababu ya kuugua mara kwa mara akiwa mahabusu,” ilikuwa ni sauti ya Jordan ambaye ilibidi aingilie kati na kumtetea Ben kwani ilionesha kama mwenyewe hawezi kufanya hivyo.
Hata hivyo, utetezi huo haukusaidia chochote, jaji alimhukumu kunyongwa hadi kufa kisha akagonga nyundo mezani na kuinuka, ukumbi wote wa mahakama ukatawaliwa na minong’ono ya hapa na pale wakati jaji na jopo lake wakitoka.
Minong’ono iliendelea, sauti za vilio pia zikawa zinasikika, hasa kutoka kwa mke wa Ben pamoja na baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa karibu. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kabisa kwa Ben ambaye uso wake uliendelea kutawaliwa na tabasamu hafifu, akawa anapunga mkono kama ishara ya kuaga wakati askari magereza wakimtoa pale kizimbani chini ya ulinzi mkali.
Waandishi wa habari nao walikuwa bize kufanya kazi yao kwani sheria zilikuwa zikiwaruhusu kuendelea kupiga picha baada ya jaji na jopo lake kutoka. Ben akatolewa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa kwenye chumba maalum kusubiria watuhumiwa wengine nao wasomewe kesi zao kisha warejeshwe gerezani.
“At last it has happened! Thanks be unto God, let your love be fulfilled!” (Hatimaye yametimia! Ahsante Mungu, mapenzi yako na yatimizwe) alisema Ben akiwa ndani ya chumba cha kusubiria, akiwa amefungwa pingu mikononi na kukalishwa chini.
Kesi ziliendelea kunguruma na baada ya washtakiwa wote kumaliza kusomewa mashtaka yao, wengine wakisomewa hukumu kama ilivyokuwa kwa Ben, walitolewa na kupelekwa kwenye karandinga chini ya ulinzi mkali.
“Ben! Nakupenda mume wangu, nisamehe kwa yote yaliyotokea, nakupenda Ben, sikuwahi kudhani unaweza kuwa unanipenda kiasi hiki,” Gladness, mke wa Ben alikuwa akisema kwa sauti ya juu, huku akilikimbilia karandinga, mwanaye akiwa mgongoni.
Ben hakuwa na cha kujibu zaidi ya kumpungia mkono kwa mbali. Japokuwa mahakamani alijikaza kiume asilie, alishindwa kuendelea kujikaza baada ya kumuona mkewe akiwa kwenye hali hiyo. Kila alipoyafikiria maisha ambayo mkewe na mwanaye wataishi baada ya yeye kufungwa, alijikuta akijisikia uchungu usioelezeka ndani ya moyo wake.
Alimfikiria pia mama yake aliyekuwa akiteseka kwa maradhi ya saratani nyumbani kwao, Maporomoko, Tunduma mkoani Mbeya kiasi cha kushindwa hata kuhudhuria hukumu ya mwanaye siku hiyo, aliwafikiria wadogo zake waliokuwa wakiteseka sababu ya umaskini, huku wote wakimtegemea yeye ndiyo awaokoe kutoka kwenye maisha ya dhiki waliyokuwa wanaishi.
“The world has let me down! I know I have let you down too! I know I have let you shed soo many tears but God will make your trespass easy! In a book of Psalm 23:3-4, its written: He restores my soul and guides me in the paths of righteousness for His name’s sake. Even though I walk through the valley of the shadow of death, I fear no evil, for you are with me…”
(Dunia imeniangusha! Najua kwamba nimewaangusha pia! Najua nimewafanya mtokwe na machozi mengi sana lakini Mungu atawafanyia wepesi katika mapito yenu! Katika kitabu cha Zaburi 23:3-4, imeandikwa: Hunihuisha nafsi yangu na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita katika bonde la kivuli cha mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami…)
Alisema Ben kwa sauti ya uchungu, machozi yakimtoka kwa wingi wakati karandinga alilopakizwa yeye na wenzake likikatiza kwenye mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, kuelekea gerezani Segerea ambako Ben angefanyiwa utaratibu na kupelekwa kwenye gereza maalum kwa ajili ya watu waliohukumiwa kunyongwa, Isanga lililopo mkoani Dodoma.

***
Agosti 13, 2002
Maporomoko, Tunduma
Kijana mdogo, Benjamini Semzaba alikuwa amekaa juu ya kiti cha miguu mitatu, chini ya kivuli cha mwembe, nje ya kibanda chao kilichojengwa kwa miti na udongo na kuezekwa kwa mabati machakavu. Mkono mmoja alikuwa amejishika tama huku mkono mwingine akiwa ameshika kitabu kidogo cha somo la Bailojia, akawa anajisomea.
Licha ya kujitahidi kuelekeza akili zake kwenye kitabu hicho, mara kwa mara mawazo machungu yalikuwa yakimpitia na kumtoa kwenye mstari, akajikuta akikifunga kitabu hicho na kukiweka chini, akajishika tama kwa kutumia mikono yote miwili, mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa chake.
“Wewe ndiyo kama baba wa hii familia, inabidi ujitahidi kuhangaika kadiri ya uwezo wako wote. Soma kwa bidii, ukipata vibarua fanya ili ndugu zako wale, mimi mama yako sina nguvu tena kama zamani, mwenyewe unajua jinsi ninavyoumwa,” kauli aliyokuwa akiambiwa mara kwa mara na mama yake ilikuwa ikijirudiarudia ndani ya kichwa chake.
Japokuwa kiumri bado alikuwa mdogo, akiwa ndiyo kwanza ametimiza miaka 16, maisha ya shida aliyokuwa akiishi na familia yake yalimkomaza na kumfanya awe na akili za kiutu uzima.
Tangu kifo cha baba yake, Tobias Semzaba, Benjamin au kwa kifupi Ben, ambaye ndiye aliyekuwa mtoto wa kwanza, alikuwa akisaidiana na mama yake kuendesha biashara ya kuuza vitumbua ambayo ndiyo iliyowafanya wamudu kuendesha maisha yao.
Kila siku asubuhi, ilikuwa ni lazima Ben awahi kuamka kuliko watu wengine wote, amsaidie mama yake kukoroga uji wa vitumbua, awashe moto kisha akamuamshe mama yake ndipo na yeye aanze kujiandaa kwenda shuleni.
Licha ya aina ya maisha waliyokuwa wanaishi, Benjamin alikuwa na ndoto nyingi kichwani mwake, ambazo zilikuwa kubwa kuliko hata yeye mwenyewe. Alikuwa na imani kubwa kwamba ipo siku atakuja kuibadilisha dunia na kuandika historia ambayo itaishi hata baada ya kifo chake.
Ndoto hizo kubwa ndizo zilizomtofautisha na vijana wengine wa rika lake, hakuona uvivu kuamka saa kumi alfajiri kila siku kwa ajili ya kuandaa mazingira ya mama yake kupika vitumbua kisha ndiyo aende shuleni. Baada ya kurudi shuleni, alikuwa akibeba vitumbua vilivyobaki mpaka muda huo na kuvitembeza mitaani kutafuta wateja.
Hakupenda kujichanganya na vijana wa rika lake kufanya mambo ya ujana. Haikuwa rahisi kumuona sehemu za starehe wala akijichanganya na wasichana. Muda wote alikuwa akipenda kujitenga peke yake, akishamaliza kuuza vitumbua, alikuwa akirudi nyumbani kwao na kama hukumkuta na kitabu, basi mkononi alikuwa na daftari akijisomea.
Biashara ya vitumbua, ndiyo iliyowezesha familia hiyo ya watoto wanne iweze kumudu kununua chakula ambacho siku nyingine, kutegemeana na jinsi biashara ilivyokuwa, walikuwa wakishindia mlo mmoja.
Ni fedha hizo ndizo zilizotumika pia kuwanunulia wote sare za shule, madaftari na vifaa vingine huku nyingine zikitumika kumlipia Ben karo shuleni kwani ni yeye peke yake ndiye aliyefanikiwa kusoma elimu ya sekondari. Hata hivyo, mtaji wa biashara hiyo ulikuwa mdogo sana kukidhi mahitaji yote, jambo lililosababisha mara kwa mara mtaji uwe unakatika. Uimara wa mama wa familia hiyo, ndiyo uliokuwa nguzo lakini kama wahenga wasemavyo, ng’ombe wa maskini hazai!
Baada ya kufanya kazi ya kupika vitumbua kwa muda mrefu, mama yake Ben alianza kulalamikia maumivu ya tumbo na kifua. Awali kila mmoja alidhani ni maumivu ya kawaida lakini kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, ndivyo mwanamke huyo alivyokuwa analalamikia maumivu ya tumbo.
Ikabidi aende hospitali ambapo vipimo vya awali vilionesha kifua chake kimepata madhara kutokana na kuvuta hewa yenye moshi kwa kipindi kirefu. Daktari akamshauri kuepuka kukaa kwenye moto, hilo likawa pigo jingine kwa familia hiyo kwani bila biashara ya vitumbua, hakukuwa na namna nyingine ya kupata fedha.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

5 Comments

Leave a Comment