Baada ya kutenda unyama wa kila aina na matukio ya kutisha, Abdulrahman anauawa na wanajeshi wa Jeshi la Umoja wa Mataifa (AMISOM) baada ya kuburuzwa kwa muda mrefu kwenye barabara ya lami. Kwa upande wa Mtima hakufahamu kabisa juu ya jambo hilo, wakati huo alikuwa katika mipango ya kumuoa msichana wa Kisukuma, Keja aliyetokea kumpenda sana.
TAMBAA NAYO…
“Kile kule ni nini?” Mtima aliyatoa macho pima na kumuuliza Keja wakiwa shambani wanaendelea na shughuli zao za kawaida.
“Mh! Sielewi.” Keja alimjibu naye akitazama kwa makini.
“Mbona ni kama kuna mtu!”
“Inawezekana, lakini atakuwa amefikaje huku?”
“Hatuwezi kujua…”
Mtima bila kutegemea, alitupa jembe chini alilokuwa ameshika mkononi na kusogea kule alikomuona mtu akiwa amelala. Keja alimfuata nyuma na walipofika walimkuta mwanamke aliyekuwa amelala chini kwenye matuta huku akionekana kuwa katika hali mbaya mno.
Alikuwa ana makovu mengi ya moto usoni na tumbo lake lilikuwa limeingia ndani jambo lililomaanisha alikuwa na njaa kali.
Kutokana na hali hiyo, Mtima na Keja walijikuta wakiingiwa na moyo wa huruma, wakaamua kumsaidia mwanamke huyo kwa kumchukua hadi alikokuwa anaishi Mtima, wakampa huduma ya kwanza pamoja na chakula baadaye akarejea katika hali yake ya kawaida kabisa.
***
Akiwa nyuma ya mawe makubwa kwenye Mapango ya Kuchungu, Destiny aliendelea kutetemeka kwa woga kutokana na mapambano aliyokuwa anayashuhudia baina ya Majeshi ya Amisom na Abdulrahman.
Moyo wake ulitulia, akapumua na kurudi katika hali ya kawaida baadaye kabisa baada ya wanajeshi hao waliotoka Somalia wakipitia Kenya hadi Mwanza, Tanzania kulikamata Kundi la Wab walikopewa taarifa na vyanzo vyao vya kijasusi kuwa ndiko lilikuwa limejichimbia, kumzidi nguvu Abdulrahman na kuondoka naye.
Baada ya kutoka kwenye maficho hayo alikokuwa amejichimbia, siku hiyo Destiny alishinda amekaa kwenye moja ya mawe makubwa yaliyokuwa katika eneo hilo huku akionekana kutawaliwa na mawazo chungu nzima hasa suala lililomchanganya zaidi kichwa chake ni wapi alikuwa Mtima maana hakufanikiwa kumuona kabisa hadi Abdulrahman anatiwa nguvuni.
Mbali na hilo, kitu kingine kilichokuwa kinamuumiza kichwa msichana huyo ni namna ambavyo angetoka katika eneo hilo kuendelea na azma yake aliyokuwa nayo ya kumtafuta Mtima.
Wakati huo hakuwa na pesa ambazo zingemsaidia kununua chochote alichokuwa anahitaji maana vitu vyake vyote vilitupwa na Abdulrahman alipomteka. Siku hiyo ilipita mwanamke huyo akiwa mwenye mawazo mengi sana lakini hadi siku tatu baadaye Destiny hakuwa ameweka tumboni kitu chochote kile.
Hali yake ikazidi kuwa mbaya, akafahamu huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, moyo wake ulimuuma mno hasa alipowaza kuwa anakwenda kufa bila kuitimiza azma aliyokuwa nayo ya kumrudisha Mtima mikononi mwake.
Destiny hakupenda kufia katika eneo hilo, aliamua kujivuta kwa nguvu zake zote kujaribu kuelekea upande ambao alihisi kungelikuwa na watu ambao wangemsaidia.
Lakini akizidi kutembea kwa shida na kujivuta ilifika hatua akahisi kuishiwa kabisa nguvu, akadondoka chini kwenye matuta na kupoteza fahamu. Baadaye alikuja kuzinduka na kujikuta akipatiwa huduma nyumbani kwa kijana mwenye ulemavu wa ngozi.
Ukweli ni kwamba muonekano wa kijana huyo ulimshitua sana Destiny baada ya kurudia kabisa kwenye hali yake ya kawaida na kushukuru kwa wema aliokuwa ametendewa. Alimtazama mara mbilimbili kijana huyo huku upande fulani wa akili yake ukimwambia huyo ndiye Mtima aliyekuwa anamtafuta, lakini mazingira aliyokuwa anaishi kijana huyo yalimfanya ajikute akipingana na mawazo hayo.
Baadaye uzalendo ulimshinda akaamua kumuuliza kijana huyo.
“Samahani kaka,” alimwambia Mtima kwa sauti ya upole.
“Bila samahani.” Mtima alimjibu.
“Kuna mtu nimekufananisha naye.”
“Nani?”
“Anaitwa Mtima.”
Baada ya kusikia kauli hiyo, Mtima alishtuka. Kwa haraka alijiuliza mwanamke huyo alikuwa ni nani mpaka aweze kumfahamu lakini hakuweza kupata jibu la moja kwa moja kutokana na muonekano wa Destiny wakati huo kuwa na mabadiliko kuliko alivyokuwa anamfahamu huko nyuma.
“Kwani wewe ni nani?” Mtima aliuliza badala ya kujibu swali ambalo Destiny alimuuliza.
“Naitwa Destiny!”
“Destiny?”
“Ndiyo, kama wewe ni Mtima tulisoma wote nchini Uholanzi.”
“Mungu wangu!”
Ukweli ni kwamba hilo lilikuwa ni jambo ambalo Mtima hakupenda kabisa kuliamini.
Je, nini kitaendelea baada ya Destiny na Mtima kukutana? Usikose Wiki ijayo!
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW
INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/
TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari
FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers
YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1