×

Rais wa China Xi: China na Marekani Zinapaswa Kuwa Washirika, Siyo Maadui

Rais wa China, Xi Jinping, ametoa wito kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kushirikiana katika kujenga mustakabali bora wa mahusiano kati ya mataifa hayo mawili makubwa duniani huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano badala ya ushindani.

Akizungumza katika mkutano wao, Xi amesema dunia kwa sasa inapitia mabadiliko makubwa huku hali ya kimataifa ikiendelea kuwa ya sintofahamu na yenye misukosuko.

“Dunia imefika katika njia panda mpya. Je, China na Marekani zinaweza kuepuka mtego huo na kuanzisha mfano mpya wa mahusiano? Je, tunaweza kukabiliana pamoja na changamoto za dunia na kuleta utulivu zaidi?” amesema Xi.

Rais huyo wa China amesema maswali hayo ni muhimu kwa historia, dunia pamoja na mustakabali wa binadamu, akieleza kuwa viongozi wa mataifa hayo wana jukumu la kutoa majibu sahihi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Xi pia ameipongeza Marekani kwa kuadhimisha miaka 250 ya uhuru wake, akisisitiza kuwa China na Marekani zina maslahi mengi ya pamoja kuliko tofauti.

“Ufanisi wa taifa moja ni fursa kwa jingine, na mahusiano thabiti kati ya China na Marekani ni jambo jema kwa dunia. Mataifa yetu yatanufaika kupitia ushirikiano na kupoteza kupitia migogoro,” amesema.

Aidha, Xi amesema anaamini China na Marekani zinapaswa kuwa washirika badala ya wapinzani, huku akieleza kuwa ushirikiano unaweza kusaidia mataifa hayo kufanikiwa na kustawi kwa pamoja katika enzi mpya.

Katika hitimisho la hotuba yake, Xi amesema anatazamia kufanya kazi kwa karibu na Trump ili kuufungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Beijing na Washington, akieleza matumaini yake kuwa mwaka 2026 unaweza kuwa wa kihistoria kwa nchi hizo mbili.

A – Z: KICHWA cha TEMBA wa IFM KILIVYOPATIKANA CHINI ya ARDHI – MGANGA wa KIENYEJI AONESHA KILIPO…

Leave a Comment