
Rais wa Marekani Donald Trump amesema yeye na Rais wa China Xi Jinping wamekubaliana kuwa Iran haipaswi kuruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia, huku wakisisitiza pia umuhimu wa kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya usafirishaji mafuta ya Strait of Hormuz.
Trump alitoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Xi mjini Beijing katika siku ya pili ya mkutano mkubwa kati ya viongozi hao wawili uliojadili masuala mbalimbali ikiwemo vita vya Iran, biashara, Taiwan pamoja na usalama wa kimataifa.
“We don’t want them to have a nuclear weapon, we want the straits open,” alisema Trump akiwa Beijing.
Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel ukiendelea kuathiri usafirishaji wa mafuta duniani baada ya Iran kufunga sehemu kubwa ya njia ya Hormuz kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanza Februari 28.

Njia hiyo ya bahari ni muhimu sana kwa biashara ya mafuta duniani kwani kabla ya vita, karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia duniani yalikuwa yakipitia katika eneo hilo.
China, ambayo ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Iran, haikutoa maelezo ya moja kwa moja kuhusu makubaliano hayo lakini wizara yake ya mambo ya nje ilisema vita hivyo “havikupaswa kutokea” na havina sababu ya kuendelea.
Trump pia alisema Xi Jinping ameahidi kuwa China haitaitumia Iran vifaa vya kijeshi, hatua ambayo imeelezwa kuwa muhimu katika kupunguza mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Iran imeendelea kusisitiza kuwa haitasitisha mpango wake wa nyuklia wala kuachia akiba yake ya uranium iliyoboreshwa, huku ikikanusha kuwa inalenga kutengeneza silaha za nyuklia.
Rais Trump ameonya kuwa uvumilivu wake unaelekea mwisho na kuitaka Iran kufanya makubaliano haraka ili kuepusha hatua nyingine za kijeshi kutoka Marekani.
Kwa upande mwingine, jeshi la Iran limeahidi kuendelea kupambana hadi tone la mwisho la damu, wakati mazungumzo ya kusitisha vita yaliyokuwa yakisimamiwa na Pakistan yakikwama baada ya Marekani na Iran kukataa mapendekezo ya kila upande.
Mgogoro huo umeendelea kuathiri usalama wa usafirishaji wa kimataifa ambapo baadhi ya meli zimeripotiwa kushambuliwa au kuzuiliwa karibu na Ghuba ya Oman na maeneo ya Falme za Kiarabu.