×

Mfadhili wa Reform UK Afichuliwa Kuwa Miongoni mwa Matajiri nchini Uingereza

Mwekezaji wa sarafu za kidijitali, Christopher Harborne, ambaye alimpatia kiongozi wa chama cha Reform UK Nigel Farage zawadi ya pauni milioni tano  sawa na Tsh Mil 17, 471,025,000 ametajwa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa nchini Uingereza katika orodha mpya ya Sunday Times Rich List 2026.

Harborne ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha hiyo akiwa nafasi ya sita, akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia pauni bilioni 18.2.

Bilionea huyo raia wa Uingereza ameishi na kufanya kazi nchini Thailand kwa zaidi ya miaka 20, huku akiwekeza katika kampuni mbalimbali za fedha na teknolojia. Miongoni mwa uwekezaji wake mkubwa ni kampuni ya Tether inayojihusisha na sarafu za kidijitali, ambayo thamani yake inakadiriwa kufikia dola bilioni 200 za Marekani.

Pia ana hisa katika kampuni ya teknolojia ya ulinzi ya Qinetiq pamoja na kampuni ya huduma za malipo ya IFX.

Harborne aliingia kwenye mjadala mkubwa wa kisiasa baada ya kumpa Nigel Farage zawadi ya pauni milioni tano mwaka 2024. Farage kwa sasa anakabiliwa na uchunguzi kuhusu iwapo alipaswa kutangaza zawadi hiyo rasmi kwa mamlaka za Bunge.

Mbali na zawadi hiyo, Harborne pia alitoa mchango mwingine wa pauni milioni tisa kwa chama cha Reform UK mwaka 2025, ukiwa mchango mkubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa chama cha siasa nchini humo na mtu binafsi aliye hai.

Orodha hiyo pia imeonyesha kupanda kwa kasi kwa utajiri wa wafanyabiashara wa teknolojia na fedha. Mwanzilishi mwenza wa Revolut, Nik Storonsky, amepanda hadi nafasi ya saba akiwa na utajiri wa pauni bilioni 16.4 baada ya thamani ya kampuni hiyo kuongezeka kwa kasi.

Aidha, mfanyabiashara Alex Gerko wa kampuni ya XTX Markets naye ametajwa kuwa na utajiri wa pauni bilioni 16.

Kwa upande mwingine, mvumbuzi maarufu Sir James Dyson na familia yake wamepoteza sehemu kubwa ya utajiri wao baada ya kushuka kwa mapato ya kampuni ya Dyson kutokana na ushuru mkubwa wa bidhaa zinazoingia Marekani.

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa idadi kubwa ya matajiri wanaondoka Uingereza kuelekea maeneo kama Dubai, Monaco na Uswisi kutokana na mabadiliko ya sera za kodi nchini humo.

Leave a Comment