×

Trump Aionya Taiwan Dhidi ya Kutangaza Uhuru wake Kutoka China

Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Taiwan dhidi ya kutangaza rasmi uhuru wake kutoka China, saa chache baada ya kumaliza mkutano wa siku mbili na Rais wa China Xi Jinping mjini Beijing.

Akizungumza katika mahojiano na Fox News, Trump alisema Marekani haitaki kuona hatua yoyote ya kuitangaza Taiwan kuwa taifa huru rasmi, akisisitiza kuwa anataka hali iliyopo sasa iendelee ili kuepusha migogoro katika eneo hilo.

“Sipo tayari kuona  Taiwan ikitangaza uhuru wake. Nataka mambo yatulie,” alisema Trump.

Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kuhusu Taiwan ukiendelea kuongezeka kati ya China na Marekani. China inaichukulia Taiwan kama sehemu ya himaya yake na imekuwa ikionya mara kwa mara kuwa inaweza kutumia nguvu kuirejesha chini ya Beijing endapo itatangaza uhuru rasmi.

Katika mkutano huo, Xi Jinping alisisitiza kuwa suala la Taiwan ndilo jambo nyeti zaidi katika mahusiano ya China na Marekani, akionya kuwa kushughulikia vibaya suala hilo kunaweza kusababisha mgongano mkubwa kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani.

Rais wa Taiwan William Ching-te Lai

Kwa upande wake, Taiwan imeendelea kusisitiza kuwa tayari ni taifa lenye mamlaka yake, huku Rais wa Taiwan Lai Ching-te akieleza hapo awali kuwa hakuna haja ya kutangaza uhuru rasmi kwa sababu wananchi wake tayari wanajiona wako huru.

Hata hivyo, Trump alisema sera ya Marekani kuhusu Taiwan haijabadilika, licha ya kuendelea kuiuzia Taiwan silaha za kujilinda. Alifichua kuwa suala la mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 11 lilijadiliwa kwa kina na Xi Jinping na bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mpango huo.

Kauli za Trump zimeendelea kuzua mjadala mkubwa kimataifa huku wachambuzi wakihofia kuwa mvutano wowote kuhusu Taiwan unaweza kuathiri usalama wa Asia na uchumi wa dunia.

Leave a Comment