
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kudhibiti upotevu wa mapato ya zaidi ya shilingi milioni 563 baada ya kubaini baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa hawalipi ushuru wa huduma kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 (Local Government Finance Act Cap 290 R.E 2019).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Elizabeth Mokiwa amesema taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji na kuwataka wafanyabiashara kulipa ushuru huo kupitia control namba za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Amesema hatua hiyo ilisababisha wafanyabiashara kuanza kulipa madeni yao ya ushuru wa huduma, ambapo jumla ya shilingi 563,663,820.15 zililipwa na kampuni mbalimbali.
“Baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wanakwepa kulipa ushuru wa huduma hali iliyosababisha upotevu wa mapato ya Halmashauri na kuathiri malengo ya ukusanyaji wa mapato,” amesema Mokiwa.

Aidha, TAKUKURU imeendesha kikao kazi na watekelezaji wa miradi mbalimbali wakiwemo wakandarasi, washauri na wasimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia maelekezo ya kiusalama kutoka TAMISEMI.
Katika kipindi hicho, TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya fedha katika miradi saba ya maendeleo. Miradi mitatu ya sekta ya afya yenye thamani ya shilingi 1,625,960,706 ni pamoja na ujenzi wa jengo la ghorofa lenye wodi ya wazazi na sehemu ya upasuaji katika Zahanati ya Ndumbwi, jengo la magonjwa ya kuambukiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni iliyopo Mabwepande pamoja na ujenzi wa uzio wa hospitali hiyo.
Pia, miradi minne ya sekta ya elimu yenye thamani ya shilingi 340,400,000 ilifuatiliwa, ikiwemo ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Makabe na Shule ya Msingi Luguruni pamoja na ujenzi wa jengo la ofisi katika Shule ya Sekondari Makabe.
Mokiwa amesema TAKUKURU pia imewafikia wananchi 6,571 kupitia semina 29, mikutano ya hadhara 26, maonesho matatu pamoja na vipindi vitano vya redio na televisheni huku klabu tisa za wapinga rushwa katika shule na vyuo zikiendelea kuimarishwa.
Kwa mujibu wa Mokiwa, jumla ya malalamiko 78 yalipokelewa katika kipindi hicho ambapo 26 yalihusu rushwa na 52 hayakuhusu rushwa. Uchunguzi wa malalamiko yanayohusu rushwa unaendelea katika hatua mbalimbali huku waliowasilisha malalamiko yasiyohusu rushwa wakipewa ushauri.
Aidha, kesi 17 zinaendelea mahakamani zikiwemo kesi mpya tatu zilizofunguliwa katika kipindi hicho. Kesi moja tayari ilitolewa hukumu ambapo Jamhuri ilishinda.
TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni imeahidi kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo, kutoa elimu ya kupinga rushwa kwa wananchi na wadau pamoja na kusimamia utekelezaji wa programu ya TAKUKURU Rafiki.
Mokiwa ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na kujiepusha na vitendo hivyo katika maeneo yao.
“Kuzuia rushwa ni jukumu letu sote; tutimize wajibu wetu,” amesema.