
Maelfu ya nyuki walizua taharuki katika Ikulu ya Marekani, White House baada ya kuvamia ghafla uwanja wa North Lawn, karibu na eneo la waandishi wa habari linalojulikana kama “Pebble Beach”.
Mashuhuda walisema kundi kubwa la nyuki lilionekana kama wingu jeusi likizunguka hewani kabla ya kuelekea kwenye mti uliopo karibu, ambapo walijikusanya na kuingia kwenye mzinga.
Tukio hilo linajiri wiki chache baada ya Melania Trump kutangaza kuongeza ‘makoloni’ mapya ya nyuki katika eneo la Ikulu hiyo, pamoja na uzinduzi wa mzinga mpya katika bustani ya South Lawn.
Haijabainika iwapo nyuki hao walivutiwa na makazi hayo mapya au walichanganya jengo hilo la kihistoria na mzinga wao mpya.
Katika vurugu hiyo, waandishi wa habari na wafanyakazi walilazimika kutawanyika kwa muda huku nyuki wakiruka kwa wingi karibu na jengo la West Wing.
Licha ya tukio hilo la kushtua, hakuna taarifa rasmi ya mtu yeyote kujeruhiwa au kudungwa na nyuki.
Mradi wa ufugaji nyuki katika Ikulu ulianza mwaka 2009 na kwa sasa unachangia uzalishaji wa asali inayotumika katika mapishi rasmi, zawadi za kitaifa na misaada ya chakula.
🐝 Tukio hilo limeacha maswali mengi kuhusu chanzo cha uvamizi huo wa ghafla, huku likionyesha pia umuhimu wa nyuki katika mazingira na uzalishaji wa chakula.