×

Waziri Mkuu Awahimiza Wananchi Kuendelea Kuiombea Tanzania

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewahimiza wananchi kuendelea kuiombea Tanzania ili amani, umoja na mshikamano wa kitaifa viendelee kuimarika sambamba na nchi kuendelea kupiga hatua za maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Amesema hayo leo Jumapili, Mei 17, 2026 aliposhiriki ibada katika (KKKT) Usharika wa Kondoa Mjini, Jimbo la Kondoa, Dayosisi ya Dodoma.

Ibada hiyo iliongozwa na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, pamoja na Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kondoa Mjini na Mkuu wa Jimbo la Kondoa KKKT .

Waziri Mkuu amesema anaendelea kushirikiana na taasisi za dini nchini akitambua mchango wake katika kujenga jamii yenye maadili, umoja na maendeleo.

“Ujumbe wake kwa wananchi wa Kondoa ni kwamba tuendelee kuiombea nchi yetu ili iendelee kuwa ya amani na kuendelea kupiga hatua za maendeleo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ikiwemo ujenzi wa daraja la kuingia Kondoa Mjini pamoja na daraja la barabara ya kuelekea Hanang.

“Tumebeba jambo la daraja la kuingia hapa Kondoa Mjini, hilo tutaanza nalo. Lakini la pili ni daraja la kuelekea Hanang ambalo na lenyewe kero yake ni kubwa sana,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mfumo wa elimu ya lazima wa miaka 10 unaotarajiwa kuanza mwaka 2028.

“Hatutakuwa na jambo linaloitwa mtoto amemaliza darasa la saba. Tunaenda kuondoa mfumo wa kuishia darasa la saba ili elimu ya lazima iwe miaka 10,” amesema.

Amesema utekelezaji wa mfumo huo unahitaji ushiriki na hamasa kutoka kwa Watanzania wote kutokana na umuhimu wa mabadiliko hayo katika sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za dini nchini.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu , kwa ushirikiano na sisi watu wa imani na viongozi wa dini,” amesema.

Aidha, amesema kanisa linaendelea kumuombea Waziri Mkuu pamoja na viongozi wa Serikali ili waendelee kulitumikia taifa kwa hekima na uadilifu.

Leave a Comment