×

Ndege Mbili za Kivita za Marekani Zagongana Angani Wakati wa Maonesho

Ndege mbili za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani aina ya Boeing EA-18G Growler zimegongana angani wakati wa maonesho ya anga yaliyofanyika karibu na kituo cha kijeshi cha Mountain Home Air Force Base, huku marubani wote waliokuwa ndani ya ndege hizo wakinusurika baada ya kujirusha nje kwa parachuti kabla ya ndege kuanguka.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili mchana wakati wa maonesho ya “Gunfighter Skies Air Show”, ambapo ndege hizo zilikuwa zikifanya maonesho ya ustadi wa kuruka mbele ya mamia ya watazamaji waliohudhuria tukio hilo.

Kwa mujibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, ndege hizo mbili zilihusika katika mgongano wa moja kwa moja zikiwa umbali wa takribani maili mbili kutoka kituo hicho cha kijeshi.

Kamanda Amelia Umayam kutoka U.S. Pacific Fleet alisema marubani wote wanne waliokuwa ndani ya ndege hizo walifanikiwa kujirusha nje salama kwa kutumia parachuti kabla ndege hazijaanguka na kulipuka.

Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha parachuti nne zikifunguka angani sekunde chache baada ya mgongano huo, huku mashuhuda wakieleza kushuhudia moshi mkubwa ukifuka kutoka eneo la tukio.

Ndege zilizohusika ni EA-18G Growler kutoka kikosi cha Electronic Attack Squadron 129 kilichopo Whidbey Island, Washington. Ndege hizo hutumika katika operesheni za “electronic warfare”, ikiwemo kuvuruga rada na mifumo ya mawasiliano ya adui wakati wa mapambano.

Baada ya ajali hiyo, waandaaji walitangaza kusitishwa kwa maonesho hayo mara moja huku eneo la tukio likizingirwa ili kuruhusu shughuli za uokoaji pamoja na uchunguzi wa chanzo cha ajali kuendelea.

Mamlaka za kijeshi nchini Marekani zimesema uchunguzi rasmi umeanza kubaini kilichosababisha ndege hizo kugongana angani.

Maonesho ya Gunfighter Skies yalikuwa yamerudi kwa mara ya kwanza baada ya kusimama kwa miaka nane tangu tukio la mwisho mwaka 2018, ambalo pia liliwahi kushuhudia ajali ya ndege iliyosababisha kifo cha rubani.

Leave a Comment