×

Wananchi Kenya Waandamana Kupinga Kupanda kwa bei ya Mafuta

Nairobi, Kenya — Wasafiri nchini Kenya wameanza kuhisi makali ya ongezeko jipya la bei ya mafuta baada ya nauli za usafiri wa umma kupanda kwa asilimia 30 kufuatia hatua ya mamlaka ya nishati kuongeza bei za mafuta kwa mwezi mmoja ujao.

Mamlaka ya Kusimamia Nishati na Petroli nchini Kenya, Energy and Petroleum Regulatory Authority (EPRA), ilitangaza kuongezeka kwa bei ya petroli kwa Shilingi 28.69 kwa lita huku dizeli ikiongezwa kwa Shilingi 40.30 kwa lita. Bei ya mafuta ya taa imeendelea kubaki ileile.

Kutokana na ongezeko hilo, Chama cha Waendeshaji wa Matatu nchini Kenya kimeongeza nauli kwa asilimia 30 kuanzia Jumatano, hatua ambayo imeibua malalamiko kutoka kwa wananchi wanaosema gharama za maisha zimezidi kuwa ngumu.

Mwenyekiti wa Chama cha Magari ya Usafiri wa Umma ya Matatu Albert Karakacha alisema gharama za uendeshaji zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na bei ya mafuta, hali inayowalazimu kuongeza nauli ili kuendelea kutoa huduma.

Wafanyabiashara wa sekta ya usafiri pia wameeleza kuwa dizeli ndiyo inayotumika zaidi katika malori na magari mazito, hivyo ongezeko hilo linaathiri moja kwa moja gharama za usafirishaji wa bidhaa nchini.

Wananchi mbalimbali wameonyesha kutoridhishwa na hali hiyo wakisema mishahara na mapato yao hayajaongezeka licha ya gharama za maisha kuendelea kupanda na kupeleka maandamono.

Katika jijini Nairobi, bei mpya za mafuta zimefikia Shilingi 206.97 kwa lita ya petroli, dizeli Shilingi 206.84 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Shilingi 152.78 kwa lita. Bei hizo zinatarajiwa kuendelea kutumika hadi mwezi ujao.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Eugene Wamalwa wameilaumu serikali kwa kuongeza mzigo kwa wananchi, wakitaka ushuru wa mafuta pamoja na VAT kupunguzwa ili kupunguza makali ya bei hiyo.

Hata hivyo, Rais wa Kenya William Ruto amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha bei ya mafuta haipandi zaidi huku akisisitiza kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta kuendesha shughuli za kiuchumi.

Leave a Comment