×

Wayne Rooney Amuita Salah ‘Mbinafsi’ Baada ya Kumkosoa Slot

Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney amemshukia vikali mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, akimuita ‘mbinafsi’ na kueleza kuwa anapaswa kuachwa nje ya kikosi kwenye mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Brentford itakayochezwa Anfield.

Kauli ya Rooney imekuja baada ya Salah kutoa maoni kuwa Liverpool inapaswa kurejea kuwa timu ya mashambulizi ya kasi na nguvu (heavy metal) inawayotisha wapinzani, aliyoyatoa baada ya kupoteza 4-2 dhidi ya Aston Villa, matokeo yaliyoacha nafasi yao ya kushiriki Ligi ya Mabingwa ikiwa mashakani.

“Ndiyo aina ya soka ninayojua kucheza na ndiyo utambulisho unaopaswa kurejeshwa na kudumishwa milele. Hili haliwezi kujadiliwa, na kila anayejiunga na klabu hii lazima ajizoeshe,” alisema katika chapisho la mitandao ya kijamii ambalo limeonekana kulenga kumkosoa Kocha Arne Slot wa Liverpool.

Mshambuliaji huyo wa Misri, Salah, 33, ataondoka Liverpool mwishoni mwa msimu baada ya kufunga mabao 257 na kusaidia klabu kushinda mataji sita makubwa ndani ya miaka tisa lakini Rooney amesema angemwacha nje katika mechi ya Jumapili ambayo pia imepangwa kutumika kumuaga rasmi Anfield.

Akizungumza kwenye kipindi chake, Rooney alisema: “Inasikitisha ukizingatia alichokifanya na mafanikio aliyopata Liverpool. Sidhani kama ilikuwa sahihi kwake kutoka hadharani na kutoa kauli nyingine ya kumkosoa Slot.

“Anataka kucheza soka la ‘heavy metal’, kwa maana nyingine anataka soka la Jürgen Klopp. Sasa sidhani kama Mo Salah anaweza kumudu aina hiyo ya soka tena. Nafikiri kasi na nguvu zake zimepungua kwa kucheza katika kiwango hicho cha juu na kasi kubwa.

“Kama ningekuwa Slot, nisingemruhusu hata kukaribia uwanja katika mechi ya mwisho. Niliwahi kupitia hali kama hiyo na Alex Ferguson.

“Tuligombana, na katika mechi yake ya mwisho Old Trafford, alinitoa kwenye kikosi kwa sababu hiyo.

“Karibu ameachia bomu na kusema hana imani na Slot, na pia amewaweka wachezaji wenzake ambao watabaki msimu ujao kwenye hali ngumu ya kukabiliana na hilo.”

🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.

Leave a Comment