
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema ameahirisha mashambulizi mapya ya kijeshi dhidi ya Iran yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumanne, kufuatia ombi kutoka kwa viongozi wa mataifa ya Ghuba huku mazungumzo mapya yakitajwa kuendelea kwa hatua nzuri.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE) walimuomba kusitisha mashambulizi hayo ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kidiplomasia.
Trump alidai kuwa ameelezwa kuwa makubaliano yanayoweza kukubalika kwa Marekani yako karibu kufikiwa, huku akisisitiza kuwa Iran haitaruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia.
Hata hivyo, rais huyo wa Marekani alionya kuwa jeshi la Marekani lipo tayari kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran wakati wowote endapo makubaliano hayo hayatapatikana.
Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Marekani, Israel na Iran ukiendelea kuongezeka tangu kuanza kwa mashambulizi makubwa ya anga mwishoni mwa Februari, ambapo Iran ilijibu kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel pamoja na vituo vya Marekani katika mataifa ya Ghuba.
Mataifa ya Ghuba yanaelezwa kuwa na hofu kubwa kuhusu uwezekano wa Iran kujibu mashambulizi zaidi kwa kulenga viwanja vya ndege, miundombinu ya mafuta na gesi pamoja na mitambo ya maji katika ukanda huo.
Wakati huo huo, Iran imeionya Marekani kuepuka kufanya “makosa ya kimkakati”, huku viongozi wa Tehran wakisisitiza kuwa wako tayari kujibu hatua yoyote mpya ya kijeshi.
Mvutano huo pia umeendelea kuathiri uchumi wa dunia baada ya Iran kuendelea kudhibiti Mlango wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta na gesi duniani, hali iliyochangia kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa.