×

Rais Samia Aitaka Afrika Kuongeza Uwekezaji wa Nishati ya Nyuklia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026. 

Rais Samia amesema Afrika inapaswa kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za nishati ili kuongeza upatikanaji wa umeme, kukuza viwanda na kuharakisha maendeleo endelevu barani humo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 19, 2026 wakati akizungumza katika Nuclear Energy Innovation Summit Africa 2026 uliofanyika mjini Kigali nchini Rwanda.

Mkutano huo wa kimataifa umewakutanisha wakuu wa nchi na serikali, wataalamu wa sekta ya nishati, wawekezaji pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa kujadili nafasi ya nishati ya nyuklia katika maendeleo ya Bara la Afrika.

Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, afya, kilimo, viwanda na tafiti za kisayansi.

Aidha, mkutano huo umejikita katika kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme Afrika, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuvutia uwekezaji katika miradi ya nishati ya kisasa.

Washiriki wa mkutano huo pia wanatarajiwa kujadili mikakati ya kukuza ubunifu wa teknolojia za nyuklia pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika na wadau wa maendeleo katika sekta ya nishati.

Kwa upande wa Tanzania, ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huo unaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za nchi kushiriki kikamilifu katika ajenda ya maendeleo ya nishati safi na endelevu barani Afrika.

Rais Samia pamoja na Viongozi mbalimbali wakishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026.
Rais Samia akitembelea maonyesho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026.
Rais Samia akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati la atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026.
Rais Samia akiwa kwenye picha na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati la Atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi mara baada ya kumaliza mazungumzo pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026.

Leave a Comment