
Klabu ya Aston Villa imefanikiwa kutwaa ubingwa wa UEFA Europa League msimu wa 2025/26 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg SC katika mchezo wa fainali uliochezwa usiku wa kuamkia leo Alhamis Mei 21, 2026 kwenye dimba la Beşiktaş Park.
Aston Villa ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 41 kupitia kwa Youri Tielemans kabla ya Emiliano Buendía kuongeza bao la pili katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili Aston Villa iliendelea kutawala mchezo ambapo Morgan Rogers alifunga bao la tatu dakika ya 58 na kuhitimisha matumaini ya Freiburg kurejea kwenye mchezo huo.
Ushindi huo umemfanya kocha Unai Emery kuendelea kuweka historia katika michuano ya Europa baada ya kuwa kocha wa kwanza kushinda taji hilo akiwa na vilabu vitatu tofauti ambavyo ni Sevilla, Villarreal na sasa Aston Villa.
Emery sasa ana mataji matano ya Europa, rekodi inayomfanya kuwa kocha mwenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya mashindano hayo baada ya kutwaa ubingwa huo mara tatu mfululizo akiwa Sevilla, mara moja akiwa Villarreal na sasa Aston Villa.