×

Rio Ferdinand Avutiwa Na Utalii Wa Serengeti, Ajionea Uhamaji Wa Nyumbu Na Simba Kwa Ukaribu

Nyota wa zamani wa Klabu ya Manchester United na timu ya Taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand akiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, wamepata nafasi ya kufanya utalii wa puto katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayotambulika duniani kwa mandhari yake ya kipekee, wanyama wengi pamoja na uzuri wa asili unaovutia maelfu ya watalii kutoka mataifa mbalimbali.

Utalii huo walioufanya leo Mei 2026, kupitia puto lililowapeleka angani, Rio Ferdinand amepata fursa ya kuona uhamaji mkubwa wa nyumbu ndani ya hifadhi hiyo, tukio ambalo ni moja ya maajabu ya dunia na moja ya vivutio vikubwa vinavyoifanya Serengeti kuwa maarufu kimataifa.

Aidha, siku ya kwanza baada ya kutua katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya hifadhi hiyo, Rio Ferdinand alipata nafasi ya kuwaona simba kwa ukaribu, jambo ambalo amesema lilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kabla ya kuwasili nchini Tanzania.

Tanzania inaendelea kujivunia kuwa miongoni mwa mataifa yenye idadi kubwa ya simba duniani, ikiwa inakadiriwa kuwa na zaidi ya simba 17,000 wanaopatikana katika hifadhi mbalimbali za taifa, hali inayochangia kukuza utalii na uhifadhi wa wanyamapori nchini.

 

Leave a Comment