
Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania, leo Mei 22, 2026 imetangaza kumuwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Tanzania Police Force (SACP), Faustine Jackson Mafwele, kwa madai ya kuhusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Marekani imesema ina taarifa za kuaminika zinazomhusisha Mafwele na vitendo vya ukandamizaji pamoja na ukiukaji wa haki za msingi za binadamu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia uchunguzi wa matukio yaliyotokea mwaka 2025, ambapo wanaharakati Agather Atuhaire wa Uganda pamoja na Boniface Mwangi wa Kenya walidai kutekwa, kushikiliwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili walipokuwa nchini Tanzania kufuatilia kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.
Kwa mujibu wa Marekani, vikwazo hivyo ni sehemu ya juhudi za kuwawajibisha watu wanaotuhumiwa kushiriki katika ukandamizaji wa haki za binadamu na kuzuia vitendo vinavyokiuka misingi ya haki na uhuru wa wananchi.
Kutokana na hatua hiyo, Mafwele hataruhusiwa kuingia nchini Marekani chini ya kifungu cha 7031(c) cha sheria ya bajeti ya usalama wa taifa na mahusiano ya nje ya Marekani.
Hadi sasa, Serikali ya Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi hawajatoa tamko rasmi kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani.