
Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes ametangazwa rasmi kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza 2025/2026 baada ya kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya timu hiyo msimu huu.
Kiungo huyo raia wa Ureno ameshinda tuzo hiyo baada ya kura zilizopigwa na mashabiki, makocha pamoja na wachambuzi wa soka, huku akiwaongoza United kumaliza ndani ya nafasi tatu za juu na kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) chini ya kocha Michael Carrick.

Fernandes aliwashinda nyota wengine waliokuwa kwenye orodha ya mwisho akiwemo Declan Rice, Gabriel Magalhães, David Raya, Erling Haaland pamoja na Morgan Gibbs-White.
Msimu huu Bruno ameonyesha kiwango cha hali ya juu baada ya kufikisha assists 20 kwenye ligi, akifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Thierry Henry msimu wa 2002/03 na Kevin De Bruyne msimu wa 2019/20. Pia amefunga mabao nane na kuhusika moja kwa moja kwenye magoli 28 ya Manchester United.

Mbali na hilo, Fernandes ametengeneza nafasi 132 za mabao msimu huu, idadi kubwa zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye ligi, akimuacha mbali Dominik Szoboszlai wa Liverpool.
Tuzo hiyo inamfanya Bruno kuwa mchezaji wa saba katika historia ya Manchester United kushinda tuzo ya Player of the Season ya Premier League, akijiunga na mastaa kama Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Nemanja Vidić ambaye alikuwa wa mwisho kuibeba mwaka 2011.
