×

Trump Aanzisha Kampeni Mpya ya Kuunganisha Israel na Mataifa ya Kiislamu

Rais wa Marekani Donald Trump.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ameziomba nchi kadhaa za Kiislamu na Kiarabu kujiunga na Makubaliano ya Abraham Accords kwa ajili ya kuhalalisha uhusiano na Israel ikiwa sehemu ya makubaliano mapya yanayotarajiwa kufikiwa na Iran.

Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema aliwasiliana na viongozi wa Saudi Arabia, Qatar, Pakistani, Misri, Jordani na Uturuki pamoja na Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain ambazo tayari ni sehemu ya makubaliano hayo tangu mwaka 2020.

Trump alisema anataka mataifa hayo kujiunga mara moja na Abraham Accords ikiwa Iran itafikia makubaliano rasmi na Marekani, akidai hatua hiyo inaweza kuunda “muungano mkubwa wa dunia” kwa ajili ya amani na ushirikiano wa kikanda.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Hata hivyo, kauli yake imeibua mjadala mkubwa kimataifa, huku wachambuzi wakieleza kuwa baadhi ya nchi alizotaja tayari zina uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Mfano, Misri na Jordan zilishasaini mikataba ya amani na Israel miaka mingi kabla ya Abraham Accords, huku Uturuki ikiwa tayari na mahusiano ya kawaida ya kidiplomasia na taifa hilo.

Kwa upande wa Saudi Arabia, chanzo kimoja kimeiambia CNN kuwa taifa hilo halitakubali kuanzisha uhusiano rasmi na Israel bila kuwepo “njia isiyoweza kubadilishwa” kuelekea kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Msimamo huo uliwahi kusisitizwa pia na Mwanamfalme Mohammed bin Salman wakati wa ziara yake mjini Marekani mwaka jana, ambapo alisema Saudi Arabia ipo tayari kujiunga na Abraham Accords lakini lazima kuwe na hatua wazi kuelekea suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina.

Leave a Comment