Marekani imefanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran baada ya kudai kugundua vikosi vya Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) vikiweka mabomu baharini katika eneo la mlango wa Hormuz karibu na Bandar Abbas, makao muhimu ya jeshi la majini la Iran.
Mashambulizi hayo yalifanyika Jumatatu usiku wa kuamkia leo Mei 26, 2026 kwa saa za Afrika Mashariki, baada ya Marekani kudai kugundua boti za IRGC zikiweka mabomu ya baharini (naval mines) katika njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa.
Kwa mujibu wa taarifa za kijeshi, Marekani ilifanya kile ilichokiita “self-defense strikes” kwa kulenga boti za IRGC pamoja na maeneo ya kuzindulia makombora karibu na Bandar Abbas. Maeneo hayo ya makombora yanadaiwa kupigwa na kuharibiwa wakati wa operesheni hiyo.

Jeshi la Marekani lilisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa lengo la kulinda wanajeshi wake, meli zake pamoja na usalama wa usafiri wa kimataifa katika Mlango wa Hormuz wakati wa kipindi cha makubaliano ya kusitisha mapigano kinachoendelea.
Ingawa IRGC haikurusha mashambulizi makubwa ya moja kwa moja, Marekani ilieleza kuwa kitendo cha kuweka mabomu baharini kilichukuliwa kama tishio la moja kwa moja kwa meli za kijeshi na biashara zinazopita katika eneo hilo nyeti duniani.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa hali katika Bandar Abbas iliendelea kuwa tulivu licha ya mashambulizi hayo yaliyoongeza mvutano mpya kati ya Iran, Marekani na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati.