Jeshi la Marekani kupitia United States Central Command (CENTCOM) limethibitisha kufanya mashambulizi ya kujilinda dhidi ya maeneo ya kijeshi kusini mwa Iran usiku wa kuamkia leo Mei 26, 2026.
Kwa mujibu wa msemaji wa CENTCOM, Kapteni Tim Hawkins, mashambulizi hayo yalilenga kulinda wanajeshi wa Marekani dhidi ya vitisho vilivyokuwa vikitokana na vikosi vya Iran.
“Vikosi vya Marekani vilifanya mashambulizi ya kujilinda kusini mwa Iran ili kulinda wanajeshi wetu dhidi ya vitisho kutoka kwa vikosi vya Iran,” alisema Hawkins katika taarifa yake.

CENTCOM imeeleza kuwa mashambulizi hayo yalihusisha maeneo ya kurushia makombora pamoja na boti za Iran zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya baharini (mines).
Mashambulizi hayo yamefanyika katika eneo la Bandar Abbas, ambako ndipo yalipo makao makuu ya jeshi la majini la Iran.
Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutajwa jina amesema operesheni hiyo ilikuwa ndogo sana kwa ukubwa wake, huku CENTCOM ikisisitiza kuwa inaendelea kuchukua tahadhari na kujizuia wakati wa usitishaji mapigano unaoendelea katika eneo hilo.
Taarifa hiyo inakuja wakati mvutano kati ya Marekani, Israel na Iran ukiendelea kuathiri usalama wa Mashariki ya Kati pamoja na shughuli za kimataifa za kijeshi na kiuchumi.