
Wimbo mpya wa Kombe la Dunia 2026 unaoitwa Dai Dai kutoka kwa Shakira akimshirikisha Burna Boy umeanza kuzua mjadala mkubwa mitandaoni huku mashabiki wengi wakilinganisha na wimbo maarufu wa mwaka 2010 Waka Waka (This Time for Africa). Wimbo huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea michuano ya Kombe la Dunia 2026 na tayari umevuta hisia kubwa kutoka kwa mashabiki wa soka na muziki duniani kote.
Video ya “Dai Dai” imehusisha mastaa wakubwa wa soka akiwemo Lionel Messi, Kylian Mbappé, Vinícius Júnior, Erling Haaland pamoja na Alexia Putellas. Video hiyo imejaribu kuonyesha umoja wa tamaduni mbalimbali kupitia burudani, dansi na mazingira ya viwanjani yaliyojaa shamrashamra za soka.
Hata hivyo, badala ya kuleta msisimko mkubwa kama ilivyotarajiwa, sehemu kubwa ya mashabiki mtandaoni wameonekana kutoridhishwa na ubora wa video hiyo huku wengi wakisema imejaa matumizi makubwa ya CGI na mandhari za green screen zilizofanya ionekane ya kutengenezwa kupita kiasi. Wapo waliodai kuwa “Dai Dai” imeshindwa kufikia hisia na mvuto uliowahi kuletwa na “Waka Waka”, ambao mpaka leo bado unatambulika kama moja ya nyimbo bora zaidi kuwahi kutumika kwenye Kombe la Dunia.
Mashabiki wengi wameendelea kujadili ikiwa Shakira aliweza kurudia uchawi alioufanya mwaka 2010 au kama “Waka Waka” bado itaendelea kubaki anthem isiyosahaulika katika historia ya mashindano hayo makubwa ya soka duniani.