
Mashabiki wa msanii wa Afrika Kusini, Tyla, wameibua taharuki mtandaoni baada ya nyota huyo kuzima akaunti zake za X na TikTok huku akiifanya akaunti yake ya Instagram kuwa ya faragha kuelekea kuachia albamu yake mpya inayotarajiwa kujulikana kama APop*.
Hatua hiyo imewaacha mashabiki wengi wakiwa na maswali mengi, hasa kutokana na muda ambao umeonekana kuwa wa muhimu katika kampeni ya kuitangaza albamu hiyo ya pili ya Tyla. Wafuasi waliokuwa tayari wanamfuatilia kwenye Instagram bado wanaweza kuona machapisho yake, lakini watumiaji wapya sasa wanatakiwa kutuma maombi ya kumfuata kabla ya kuona maudhui yake.
Baadhi ya mashabiki wameeleza kuwa huenda Tyla ameamua kupumzika kutoka kwenye mitandao ya kijamii kutokana na maneno makali na ukosoaji anaokumbana nao mara kwa mara mtandaoni, huku wengine wakiamini hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kutangaza albamu yake mpya.

Mtumiaji mmoja wa X aliyejitambulisha kama BrunoSingwela aliandika kuwa ana matumaini Tyla atarejea akiwa imara zaidi, akisema si rahisi kwa mtu maarufu kusoma maneno mabaya anayosemwa kila siku mtandaoni.
Hatua ya Tyla imeendelea kuzua mijadala mikubwa miongoni mwa mashabiki wake maarufu kama “Tygers”, ambao sasa wanaendelea kufuatilia kwa karibu kuona iwapo kutakuwa na tangazo rasmi kuhusu albamu hiyo au kurejea kwake kwenye mitandao ya kijamii.