
Marekani usiku wa kuamkia leo Mei 28, 2026 imefanya mashambulizi mapya mara ya pili ndani ya siku tatu nchini Iran karibu na mlango wa bahari wa Hormuz, huku Rais wa Marekani, Donald Trump akipinga taarifa za mpango wa amani kati ya nchi yake na Iran akizitaja kuwa uzushi.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mashambulizi hayo yalilenga kituo cha kudhibiti ndege zisizo na rubani (drone) katika mji wa Bandar Abbas ambacho kilidaiwa kuwa tishio kwa majeshi ya Marekani pamoja na meli za biashara zinazopita katika eneo hilo muhimu la usafirishaji wa mafuta duniani. Marekani pia ilisema imefanikiwa kudungua drone nne za Iran zilizokuwa zikielekea katika eneo la Strait of Hormuz.
Mashambulizi hayo yamekuja wakati mazungumzo ya kutafuta suluhu ya vita kati ya Iran, Marekani na Israel yakiendelea, huku mvutano ukiongezeka kuhusu usalama wa njia ya bahari ya Hormuz ambayo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta duniani.

Iran kupitia Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) ilidai kujibu mashambulizi hayo kwa kulenga kambi ya jeshi la Marekani mapema Alhamisi, huku ikionya kuwa mashambulizi yoyote yajayo yatakabiliwa na majibu makali zaidi. Serikali ya Kuwait pia ilithibitisha kuwepo kwa mashambulizi ya makombora na drone katika eneo la Ghuba ya Uajemi bila kutaja yalipotokea.
Katika mkutano wa Baraza la Mawaziri Ikulu ya Marekani, Trump alikanusha taarifa zilizorushwa na televisheni ya taifa ya Iran zilizodai kuwa Marekani na Iran zimefikia rasimu ya makubaliano ya amani yatakayoruhusu kufunguliwa tena kwa Strait of Hormuz pamoja na kuondolewa kwa vizuizi vya kijeshi vya Marekani.

Trump alisema Marekani “haijaridhishwa” na mapendekezo ya Iran na kuongeza kuwa iwapo makubaliano hayatapatikana, Marekani inaweza “kumaliza kazi”. Pia alisisitiza kuwa hakuna taifa litakalodhibiti njia ya Hormuz akisema njia hiyo ni ya kimataifa na lazima ibaki wazi kwa mataifa yote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema kuna dalili za maendeleo katika mazungumzo hayo lakini bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili.
Mvutano huo umeendelea kuathiri soko la mafuta duniani ambapo wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa hali ikiendelea, bei za mafuta na gharama za maisha zinaweza kuongezeka zaidi katika mataifa mbalimbali duniani.
