
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, ndugu na wananchi wamehudhuria mazishi ya marehemu Bi. Suzana Ngolo Magufuli yaliyofanyika leo Mei 29, 2026 katika eneo la Kilimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Mwili wa marehemu Bi. Suzana Magufuli ambaye ni mama mzazi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli umeshushwa kaburini huku waombolezaji wakitoa heshima zao za mwisho katika mazishi hayo yaliyogubikwa na huzuni kubwa.

Viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti walikusanyika Chato kushiriki ibada na shughuli za mazishi ya mama huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika familia ya Hayati Dkt. Magufuli.
Mazishi hayo yamefanyika kwa heshima kubwa huku salamu za pole zikiendelea kutolewa kwa familia ya marehemu pamoja na wananchi wa Chato.
