
Msanii nyota kutoka Afrika Kusini Tyla anatajwa kuungana na rapa maarufu wa Marekani Future kwenye wimbo mpya wa Kombe la Dunia 2026 unaoitwa Game Time.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali pamoja na video za utambulisho zilizosambaa mtandaoni, wimbo huo unatarajiwa kuachiwa rasmi Mei 29 ikiwa sehemu ya kampeni ya muziki kuelekea mashindano ya FIFA World Cup 2026 yatakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Ushirikiano huo umeibua msisimko mkubwa kutokana na mchanganyiko wa muziki wa amapiano-pop wa Tyla pamoja na mtindo wa trap wa Future, jambo ambalo mashabiki wengi wanaamini linaweza kuzaa wimbo mkubwa wa kimataifa.

Tyla ambaye aliuteka ulimwengu kupitia hit yake Water, anaendelea kupanda kimataifa na sasa ametajwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza kwenye sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 sambamba na majina makubwa kama Katy Perry, LISA, Rema na Anitta.
Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea yakishirikisha timu 48 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Ripoti zinaeleza kuwa FIFA inalenga kujenga kampeni kubwa ya muziki kwa mashindano hayo badala ya kutegemea wimbo mmoja pekee wa mashindano. Tayari wasanii kama Shakira, Burna Boy, Daddy Yankee na Shenseea wamehusishwa na nyimbo mbalimbali za kuelekea mashindano hayo.
Mitandao ya kijamii imeendelea kulipuka kwa maoni ya mashabiki wengi hasa kutoka Afrika wakieleza fahari yao kumuona Tyla akiwa sehemu ya kampeni kubwa ya muziki wa Kombe la Dunia.