
Los Angeles, Marekani — Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Jimbo la Los Angeles (D.A.) inaendelea kufanya mapitio ya kesi mpya inayomhusisha rapa na mogul wa muziki Sean Combs kufuatia madai ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyowasilishwa na publicist Jonathan Hay.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari, Jonathan Hay alifungua ripoti ya polisi Septemba 2025, akidai matukio mawili ya unyanyasaji yaliyotokea mwaka 2020 na 2021. Kesi hiyo awali ilifunguliwa Florida kabla ya kuhamishiwa Los Angeles ambako inadaiwa matukio hayo yalitokea.
Inaripotiwa kuwa wapelelezi wa polisi wa LAPD walifanya uchunguzi kwa miezi kadhaa kabla ya kuwasilisha majumuisho yao kwa ofisi ya D.A., ambayo sasa inaamua kama kuna ushahidi wa kutosha kufungua mashtaka rasmi dhidi ya msanii huyo.

Jonathan Hay anadai kwamba matukio hayo yalitokea wakati akiwa anashirikiana kwenye mradi wa muziki unaohusisha CJ Wallace, mtoto wa marehemu rapa Christopher “Biggie Smalls” Wallace, ambapo Diddy alikuwa na uhusiano wa karibu na familia hiyo kutokana na historia yake ya ushirikiano na Biggie.
Kwa upande wake, hadi sasa upande wa Sean Combs haujatoa majibu rasmi kuhusu tuhuma hizo mpya.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2025, Diddy alihukumiwa katika mahakama ya shirikisho kwa kosa la kusafirisha watu kwa ajili ya shughuli za ngono, lakini aliachiliwa huru katika mashtaka mengine mazito zaidi kama vile usafirishaji wa binadamu na uendeshaji wa mtandao wa uhalifu.
Kwa sasa, D.A. wa Los Angeles anaendelea kuchambua ushahidi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatua za kisheria zitakazofuata.