×

Rais Samia Aelekea Urusi Kwa Ziara ya Siku Tatu, Kufungua Fursa Mpya za Uwekezaji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka nchini, kuelekea Shirikisho la Urusi kwa ziara ya Kitaifa itakayoanza tarehe 3 hadi 5 Juni, 2026 kwa mualiko wa Rais wa Shirikisho la Urusi, Mheshimiwa Vladimir Putin

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameondoka nchini kuelekea Shirikisho la Urusi kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu itakayofanyika kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026 kwa mwaliko wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Rais Samia ameondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ambapo ameagwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika ziara hiyo, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin kuhusu kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara, uwekezaji pamoja na ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo kati ya Tanzania na Urusi.

Aidha, Rais Samia pia atashiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF), ambalo hukutanisha viongozi wa mataifa, wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kujadili masuala ya uchumi na maendeleo ya kimataifa.

Ziara hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Tanzania kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia uwekezaji pamoja na fursa mpya za maendeleo kwa Taifa.

Leave a Comment