×

RC Makalla Azindua Kamati 7 Maandalizi ya Mkutano wa IPU Arusha


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla amezindua kamati saba za Mkoa ambazo zitawajibika kusimamia maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaokutanisha Nchi 183 Mkoani hapa, Akisisitiza maandalizi na hamasa nzuri pamoja na kuufungamanisha Mkutano huo na sekta ya Utalii, biashara na Uwekezaji wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.

“Tanzania imepata heshima kubwa kati ya Nchi zote 183 zilizopo IPU, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepata heshima hiyo, Mkoa wa Arusha umepata heshima hiyo- kwahiyo sisi Mkoa wa Arusha kama mwenyeji lazima tuhakikishe tunafanya maandalizi makubwa na hamasa kubwa ya kukumbukwa na Wabunge wa IPU, hatutoifanya kinyonge, tunataka dunia ituelewe, dunia ielewe Arusha ni kitovu cha utalii, tunataka dunia ielewe Tanzania ni Nchi ya aina gani. Hii ni fursa pia kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha katika sekta ya utalii, usafirishaji, malazi na chakula.” Amesema Makalla.

Akizungumza na sehemu ya wajumbe wa Kamati hizo leo Jumanne Juni 02, 2026, Ofisini kwake Jijini Arusha, Mhe. Makalla amezitaja Kamati hizo kuwa ni Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Itifaki na Mapokezi, Kamati ya Malazi na Usafiri, Kamati ya Ukumbi na Mapambo, Kamati ya Habari, Mawasiliano na Hamasa, Kamati ya Burudani, Utamaduni na Utalii pamoja na Kamati ya Afya na Chakula.

Katika maelezo yake Mhe. Makalla amesema kuelekea katika Mkutano huo mwezi Oktoba mwaka huu amezitaka kamati hizo kuandaa na kuratibu vikao mbalimbali na wananchi na wadau wanaohusika na Kamati hizo ikiwemo wenye Hoteli, Madereva Tax, wenye nyumba za kukodisha (AirBnB) na wenye Makampuni ya utalii ili kuwaeleza kuhusu fursa za ujio wa mkutano huo na namna ya kuweza kuzifikia na kuzitumia kikamilifu.

Makalla amebainisha kuwa tamanio lake baada ya Mkutano huo mkubwa ni kuona washiriki wa mkutano huo wanaondoka Nchini kwa furaha ili iwe kama mtaji muhimu wa wao kurejea nchini kwa shughuli za utalii na uwekezaji, akisisitiza furaha, hamasa na usalama katika Mkutano huo na bila ya kubugudhi wageni, watalii na wananchi wa Mkoa wa Arusha wakati wote wa Mkutano huo.

Leave a Comment