
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema msaada wa kijeshi kutoka Marekani ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote baada ya Urusi kufanya moja ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya Ukraine katika miezi ya hivi karibuni.
Akizungumza Jumanne, Zelensky amesema mashambulizi hayo ya usiku yaliyohusisha makombora na ndege zisizo na rubani (drones) yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 18 huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.

“Ulaya inahitaji mfumo wake wa ulinzi dhidi ya makombora ya ballistic ili vita hivi viweze kumalizika,” amesema Zelensky. “Msaada wa Marekani katika kusambaza makombora ya mfumo wa Patriot ni muhimu kabisa.”
Kwa mujibu wa Zelensky, Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 656 pamoja na makombora 73 ya aina mbalimbali kuelekea Ukraine katika mashambulizi hayo makubwa yaliyolenga zaidi mji mkuu wa Kyiv na mji wa Dnipro.
Maafisa wa Ukraine wamesema watu sita wamefariki mjini Kyiv huku zaidi ya watu 70 wakijeruhiwa baada ya majengo ya makazi na miundombinu mingine ya kiraia kuharibiwa vibaya.

Katika mji wa Dnipro, watu 12 wanadaiwa kupoteza maisha huku zaidi ya watu 30 wakijeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo.
Kampuni ya nishati ya Ukraine, DTEK, imesema mashambulizi hayo yalisababisha zaidi ya wakazi 140,000 wa Kyiv kukosa umeme kwa muda kabla huduma hiyo kurejeshwa kwa sehemu kubwa ya maeneo yaliyoathirika.
Aidha, kampuni ya mafuta na gesi ya Ukraine, Naftogaz, imethibitisha kuwa moja ya miundombinu yake muhimu katika eneo la Kharkiv ilipigwa na mashambulizi hayo.

Mkurugenzi Mkuu wa Naftogaz Group, Sergii Koretskyi, amesema mashambulizi hayo ni sehemu ya mbinu za Urusi za kusababisha madhara makubwa kwa miundombinu pamoja na watu wanaoshiriki shughuli za uokoaji na ukarabati.
Jeshi la anga la Ukraine limeeleza mashambulizi hayo kuwa ni “shambulio kubwa la anga,” likidai Urusi ilitumia zaidi ya malengo 700 ya anga ikiwemo drones aina ya Shahed na makombora ya ballistic.
Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mashambulizi hayo yalikuwa ni kulipiza kisasi dhidi ya kile ilichodai kuwa ni mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine katika eneo linalodhibitiwa na Urusi mashariki mwa Ukraine.

Mvutano huo mpya unakuja huku Zelensky akiendelea kuishinikiza Marekani pamoja na washirika wa Magharibi kuongeza mifumo ya ulinzi wa anga na vikwazo zaidi dhidi ya Moscow.
Wiki iliyopita, Zelensky alimtumia barua Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na wajumbe wa Bunge la Marekani akiomba msaada zaidi wa mifumo ya ulinzi wa anga.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, naye ametoa wito kwa washirika wa Ukraine kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Urusi, akisema juhudi za amani haziwezi kufanikiwa bila kuongeza shinikizo dhidi ya Moscow.