
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema angependa kukutana na kiongozi wa juu wa Iran, Mojtaba Khamenei, huku akibainisha kuwa huenda mkutano huo ukafanyika siku zijazo kulingana na maendeleo ya mazungumzo ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la New York Post kupitia kipindi chake cha “Pod Force One,” Trump alisema kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaendelea na kuna matumaini ya kufikia makubaliano kuhusu suala la silaha za nyuklia.
Trump alidai kuwa Iran tayari imekubali kutotengeneza au kumiliki silaha za nyuklia, akisema hatua hiyo ni sehemu ya mazungumzo yanayoendelea kati ya pande hizo mbili.

Katika mahojiano hayo, pia alizungumzia hali ya kisiasa Mashariki ya Kati, hasa mzozo kati ya Israel na Lebanon, akisema hakufurahishwa na namna mapigano hayo yanavyoendelea.
Ingawa alieleza kuwa wakati fulani alikuwa amekasirishwa na hatua za Israel, Trump alisisitiza kuwa bado ana uhusiano mzuri na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Hata hivyo, ripoti za vyombo vya habari, zikiwemo Axios, zilidai kuwa katika mazungumzo ya simu na Netanyahu, Trump alitumia maneno makali kumkosoa kuhusu mwenendo wa vita, ingawa hakuthibitisha kikamilifu kauli hizo katika maelezo yake.
Trump alisema amemwambia Netanyahu kuwa ni muhimu kusitisha mapigano, akisisitiza haja ya kutafuta suluhu ya haraka kwa migogoro hiyo inayoendelea.