×

Makamu wa Rais Ahimiza Ushirikiano Katika Uhifadhi wa Mazingira (Picha +Video)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito wa kutumia Maadhimsho ya Siku ya Mazingira Duniani kukumbuka wajibu wa kuunganisha nguvu katika jitihada za kuhifadhi mazingira, na kuhakikisha matumizi adili ya rasilimali nyingi ambazo Tanzania imejaaliwa kuwa nazo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, ambayo Kitaifa yamefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Amesema baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia katika uhifadhi wa mazingira ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya mazingira na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka hususan katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa dhana ya uchumi rejeshi, kwa kuwa maeneo mengi bado hali ya usafi haridhishi.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba, ni vema kuendelea kubadili mtazamo ili kuziona taka kama fursa ya kiuchumi na kuzitumia kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile mbolea, chakula cha mifugo na bidhaa nyinginezo. Hali kadhalika, kuendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo hadi sasa, matumizi hayo yameendelea kuimarika kutoka 6.9% mwaka 2021 hadi kufikia 28.6% mwaka 2025.

Aidha, Makamu wa Rais amehimiza kuongezwa kwa jitihada za uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambapo ameagiza Mamlaka zinazotoa vibali vya ujenzi kuweka sharti na kusimamia ili kila kibali cha ujenzi kinachotolewa kinaambatana na agizo la kupanda miti isiyopungua mitano pamoja na kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan Manispaa na Majiji kuazisha Bustani za kijani na kuhakikisha zinatunzwa ipasavyo.

Pia Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuhakikisha uwepo wa miche ya miti ya kutosha ili kurahisisha na kuwezesha zoezi la upandaji miti nchini, Mamlaka husika kuimarisha udhibiti wa uharibifu wa maeneo yote yanayopandwa miti pamoja na kuiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia kituo cha Taifa cha kuratibu kaboni kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), kubainisha misitu inayofaa na kuisajili katika biashara ya kaboni.

Leave a Comment