
Jeshi la Marekani limesema limeangusha ndege nne zisizo na rubani (drones) za Iran zilizokuwa zikielekea katika Mlango wa Bahari wa Hormuz siku ya Ijumaa, kabla ya kushambulia baadhi ya vituo vya rada vya Iran kujibu mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), drones hizo zilikuwa tishio la moja kwa moja kwa usafiri wa meli katika eneo hilo muhimu kwa biashara ya kimataifa.
“Drones hizo zilikuwa tishio la haraka kwa usafiri wa majini katika ukanda huo,” CENTCOM ilisema kupitia mtandao wa kijamii.
Jeshi hilo lilisema baadaye lilifanya mashambulizi dhidi ya vituo vya rada vya ufuatiliaji wa pwani katika maeneo ya Goruk na Kisiwa cha Qeshm ili kuzuia mashambulizi zaidi kutoka Iran.
Awali, CENTCOM ilikanusha madai ya Iran kwamba jeshi lake lilifyatua risasi za onyo dhidi ya meli za kivita za Marekani katika Ghuba ya Oman na kuzilazimisha kurejea kuelekea Bahari ya Hindi.
“Vikosi vya Marekani vinaendelea kufanya operesheni kwa uhuru katika maji ya ukanda huo huku vikitekeleza kikamilifu mzingiro dhidi ya Iran,” CENTCOM ilisema.
Marekani imeendelea kuweka mzingiro dhidi ya bandari za Iran kufuatia kile ilichokiita juhudi za Tehran kudhibiti njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi asilia duniani kupitia Mlango wa Hormuz, jambo lililosababisha kupanda kwa bei za nishati na kuongeza presha za kisiasa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuelekea uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula.
Katika hatua nyingine, Trump alisema hali ya Iran “inaonekana kwenda vizuri” licha ya mashambulizi hayo kuibua hofu mpya kuhusu kusambaratika kwa usitishaji vita uliopo.
“Tutatoka kwenye suala la Iran haraka sana na litakuwa jambo lenye nguvu kwa namna moja au nyingine, iwe kwa makubaliano ya karatasi au kwa njia ngumu zaidi,” Trump alisema akiwa kwenye hafla ya wakulima mjini Wisconsin.
Trump pia alisema Iran bado ina asilimia 21 hadi 22 ya hifadhi yake ya makombora.
Wakati huo huo, mapigano katika Lebanon yanaendelea kuongeza mvutano wa ukanda huo baada ya jeshi la Israel kushambulia maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon, huku kundi la Hezbollah likikataa makubaliano ya usitishaji vita yaliyojadiliwa kwa ushirikiano wa Marekani.
Aidha, jeshi la Marekani lilisema limekamata tanker moja ya mafuta inayohusishwa na Iran katika Bahari ya Hindi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia Iran kunufaika kupitia biashara ya mafuta.
Marekani pia imeweka vikwazo vipya dhidi ya sekta ya nishati ya Iran, ikilenga watu, kampuni na meli zinazohusishwa na biashara hiyo.