×

Marubani Wawili Wafariki Katika Ajali ya Private Jet ya Yadier Molina

Gwiji wa zamani wa mchezo wa Baseball, Yadier Molina amenusurika kupanda ndege binafsi aina ya Gulfstream G200 iliyopata ajali na kulipuka moto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa La Romana International Airport nchini Dominican Republic.

Ndege hiyo iliripotiwa kuanguka Juni 8, 2026 wakati ikitua kwa dharura, na kusababisha vifo vya marubani wawili raia wa Marekani waliokuwa ndani yake pekee. Marubani hao walikuwa wakielekea kumchukua Molina pamoja na familia yake na marafiki zake kwa safari ya kuelekea Texas, nchini United States.

Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Jamhuri ya Dominika, ndege hiyo ilikuwa imeondoka Puerto Rico kabla ya kutua La Romana kwa ajili ya kujaza mafuta na kuendelea na safari kuelekea mji wa Austin.

Taarifa mbalimbali zilizochapishwa mitandaoni zimemnukuu Molina akithibitisha kuwa ndege hiyo ilikuwa imepangwa kumbeba yeye, familia yake pamoja na marafiki zake. Ndege hiyo yenye usajili wa N318JF ilikuwa na uwezo wa kubeba hadi abiria 18.

Wakati huo huo, uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea chini ya mamlaka husika za anga za Dominican Republic, huku video zilizosambaa mitandaoni zikionesha ndege hiyo ikitua ikiwa na hitilafu inayodaiwa kuhusisha matairi ya nyuma kutokuonekana vizuri kabla ya kulipuka moto.

Leave a Comment