×

Kamanda Muliro Aeleza Watuhumiwa wa Mauaji Raia wa China Walivyokamatwa

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Muliro J. Muliro amesema kuwa wananchi wanakumbuka kwamba tarehe 16 Mei, 2026, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lilianza uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya mtu aliyefahamika kwa jina la Bhaozan Li, raia wa China na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa kiitwacho XIL LI, kilichopo eneo la Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam, ambaye aliuawa kikatili na watu waliodaiwa kuwa walinzi wa kiwanda hicho.

Amesema baada ya upelelezi wa kina uliohusisha mamlaka za kiuchunguzi za Jeshi la Polisi, watuhumiwa wanne wamekamatwa katika maeneo tofauti kuhusiana na tukio hilo la mauaji.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walihojiwa kwa kina kwa kuzingatia mifumo ya kisheria na wamekiri kula njama kwa pamoja za kumvamia usiku, kumshambulia na baadaye kumuua mtu huyo, kisha kuiba fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tisa zilizokuwa ndani ya kiwanda hicho.

Ameeleza kuwa mara baada ya kutekeleza tukio hilo, watuhumiwa walitoroka na baadaye kukamatwa katika maeneo ya Namanga mkoani Arusha na Mabibo jijini Dar es Salaam kwa siku tofauti tofauti ambapo watuhumiwa hao ni:

  1. Godson Simon maarufu Laizer (25), mkazi wa Olkolili, Siha, Kilimanjaro.
  2. Elisha Saitoti maarufu Luqmay (24), mkazi wa Mkonde, Handeni, Tanga.
  3. Godfrey Laban maarufu Mollel (30), mkazi wa Makongo, Kinondoni.
  4. Godson Pineli maarufu Lisika (24), mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa wote watafikishwa kwenye mamlaka nyingine za kisheria haraka iwezekanavyo.

Aidha, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limetoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kihalifu, likisisitiza kuwa uhalifu huwaingiza wahusika katika msuguano mkubwa wa kisheria.

Leave a Comment