×

Serikali Yapendekeza Kupunguza Kodi za Magari ya Umeme na Vifaa vya Nishati Safi – Video

Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imependekeza hatua mbalimbali za kikodi zitakazochochea matumizi ya nishati safi ikiwemo umeme na gesi asilia nchini.

Akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Khamis alisema Serikali inapendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vinavyotumika katika vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme vinavyoingizwa nchini.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kuchaji magari ya umeme na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Mbali na hilo, Serikali imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kwa magari yanayotumia nishati ya umeme kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10. Pendekezo hilo linatarajiwa kupunguza gharama za uingizaji wa magari hayo na kuyafanya yafikike kwa wananchi wengi zaidi.

Waziri Khamis alisema Serikali pia inaendelea na majadiliano na viwanda vya kuunganisha magari vilivyopo nchini ili kuandaa utaratibu wa kutoa unafuu wa kodi kwa waunganishaji wa magari ya umeme, hatua ambayo inaweza kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha sekta ya viwanda.

Katika jitihada za kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali imependekeza kusamehe VAT kwenye mita janja za gesi ya mitungi ya kupikia (LPG Smart Meter) zinazoingizwa nchini.

Alifafanua kuwa msamaha huo utatolewa kwa wasambazaji wa gesi ya kupikia pekee, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za gesi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi majumbani.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhamia kwenye matumizi ya nishati endelevu, kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kijani nchini.

Leave a Comment