×

Serikali Kuongeza Ushuru wa Kamari Kufikia 5% Kupunguza Madhara ya Kijamii

Serikali imependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye thamani ya dau la kamari zinazochezwa kupitia michezo ya kubashiri ya mtandaoni na ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kasino, mashine za sloti na michezo ya vikaragosi (virtual games).

Akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti ongezeko la uraibu wa kamari hususan miongoni mwa vijana.

Waziri Khamis alisema Serikali ina wasiwasi kuwa kuongezeka kwa michezo ya kubahatisha kumesababisha baadhi ya vijana kupoteza muda na nguvu kazi inayoweza kutumika katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya taifa.

Aidha, amesema asilimia 10 ya mapato yatakayokusanywa kutokana na ushuru huo wa asilimia 5 yataelekezwa kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) ili kusaidia kuboresha usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Serikali, hatua hiyo haitalenga tu kudhibiti athari za kijamii bali pia kuongeza mapato ya taifa, ambapo inakadiriwa Serikali inaweza kukusanya takribani shilingi bilioni 74.50 kupitia ushuru huo mpya.

Waziri Khamis amesema mapendekezo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha sekta ya michezo ya kubahatisha inasimamiwa kwa ufanisi huku ikizingatia ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

Leave a Comment